Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ulega: Uhitaji wa nyama umeongezeka, sekta imekua

98e4b7984ac3e69356a70ea96de7d721 Ulega: Uhitaji wa nyama umeongezeka, sekta imekua

Wed, 20 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema malalamiko yaliyojitokeza hivi karibuni ya kupanda kwa bei ya nyama nchini yanaashiria ukuaji wa sekta hiyo ambapo wafugaji wameshauriwa kuwa huu ni muda mzuri kwa wao kuvuna na kuuza mifugo yao.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amebainisha hayo leo Oktoba20, 2021 jijini Dodoma, mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Nyama nchini mbele ya kamati hiyo.

Ulega amesema kipindi cha nyuma wafugaji walikuwa wakilalamika kutopata masoko ya mifugo yao ila katika kipindi cha sasa uhitaji wa mifugo katika viwanda vya kuchakata nyama nchini umekuwa mkubwa pamoja na hitaji la nyama katika soko la ndani.

“Sekta ambayo ulikuwa hauwezi kuisikia inasemwa, lakini leo inakuwa mjadala hivyo ni wakati mzuri sana kwa wafugaji kuvuna na kuuza mifugo yao.” amesema Ulega

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dk Daniel Mushi, ameiambia kamati hiyo kuwa uhaba wa nyama uliojitokeza hivi karibuni na kusababisha bei ya nyama kupanda ni fursa ya kufuga kibiashara na kunenepesha mifugo hiyo.

Amesema serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu, imetengeneza uhitaji wa nyama baada ya kufungua biashara ya kuuza nyama nje ya nchi hivyo uhitaji wa mifugo kwenye viwanda vya kuchakata hapa nchini umeongezeka.

Ameongeza kuwa hivi karibuni Tanzania kupitia viwanda vilivyopo nchini itaanza kupeleka nyama katika soko la Saudi Arabia na kwamba hitaji la soko hilo ni Tani Laki Sita kwa mwaka hali ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya mifugo nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz