Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ulaghai mtandaoni mfupa mgumu, wachumi watoa tahadhari

Hacker In Mask And Hood Account Hacking 2021 08 26 16 25 33 Utc Scaled 1 1140x640 Ulaghai mtandaoni mfupa mgumu, wachumi watoa tahadhari

Sun, 4 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kampuni za huduma za simu, bado ulaghai mtandao ni changamoto kubwa inayowakumba maelfu ya wananchi.

Ripoti ya TCRA ya robo ya nne ya mwaka 2023 iliyotoka mwanzoni mwa wiki hii, inaonyesha kuwapo kwa matukio 21,788 ya ulaghai katika kipindi cha miezi 3 (Oktoba, Novemba na Desemba).

Kama ilivyo katika ripoti zilizopita mikoa mitatu ya Rukwa yenye laini zilizo hai milioni 1.1, Morogoro milioni 3.5 na Dar es Salaam milioni 12.9 inaongoza kwa visa vingi vya ulaghai, huku mikoa ya Kaskazini Pemba yenye laini 108, 600 na Kusini Pemba laini 108,640 ikiwa na visa chini ya kumi.

Katika kipindi husika mikoa mitano iliyoongoza kwa kuwa na visa vingi ni Rukwa ambao umeripotiwa kuwa na visa 7,666, Morogoro visa 7,171, Dar es Salaam visa 1,717, Mbeya visa 1,549, Tabora visa 590.

Kwa jumla mikoa hiyo ilichangia zaidi ya asilimia 83 ya visa vyote.

“Kuna wakati matukio huwa yanakata unamaliza hata mwezi hujatumia zile meseji zao za tuma kwa namba hii lakini unashangaa zinaibuka tena, unaripoti lakini wanabadili tena namba,” amesema Mariam Andilo, mkazi wa Sinza, Dar es Salaam.

Wakizungumzia juhudi wanazozifanya kudhibiti ulaghai huo, TCRA wanasema wameanza kuyaona matunda ya kile wanachokifanya baada ya idadi ya laini zinazofungwa kufuatia matukio hayo kuendelea kupungua.

Jumla ya laini 30,309 zilifungiwa katika robo ya nne ya mwaka 2023 ulioishia Desemba ikilinganishwa na laini 34,848 zilizofungiwa katika robo ya tatu ya mwaka 2023 ulioishia Septemba, taarifa ya TCRA inayochambua robo ya mwisho wa mwaka 2023 inaeleza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TCRA, Dk Jabir Bakari kufungiwa kwa laini hizo kunasaidia kupunguza matukio ya wizi.

"Hii pi, inasaidia upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano vyenye ubora kwenye soko," amesema Dk Jabir.

Amesema juhudi za kukabiliana na simu za ulaghai na zinazotumika kwa utapeli zinaelekea kuzaa matunda kutokana na kupungua kwa matukio yaliyoripotiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, visa vya ulaghai vimeshuka kutoka asilimia mbili ya idadi ya laini za simu zilizokuwa zimesajiliwa hadi Septemba, 2022 kufikia asilimia 0.01 Desemba 2023.

"Simu za ulaghai zilianza kupungua Novemba 2022. Pia, simu zilizofungiwa baada ya kuripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu pia zilipungua kwa asilimia 13.03 kati ya Septemba na Desemba 2023," imeelezwa.

Hilo lilienda sambamba na ufungaji wa namba tambulishi baada ya kuripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu ambazo nazo zilishuka kwa asilimia 13.

Hata hivyo, matumaini ya watu ilikuwa ni kuona jambo hilo linaisha kutokana na juhudi ambazo zinatangazwa na kampuni zinazotoa huduma, TCRA na kiama kilichotangazwa na Waziri Bungeni.

Kauli ya Nape

Mei mwaka jana akijibu maswali Bungeni, Waziri Nape Nnauye alisema idadi ya laini imekuwa kubwa kuliko idadi ya Watanzania hivyo katika mazingira hayo wahalifu wamo akitumia msemo wa, “kwenye msafara wa mamba na kenge wamo.”

“Mwanzoni usajili wa laini ulikuwa unafanyika holela, mtu anakamatwa lakini unakuta sio yeye aliyesajili laini hivyo kesi inaishia hapohapo, mkienda mahakamani akikuruka inaisha, tulichokifanya tukazisajili laini zile kwa alama za vidole lakini utapeli ukaendelea,” alisema.

Alisema baada ya hapo ukafanyika uhakika ambao ulihakikisha sasa kila namba inamilikiwa na mwenyewe jambo ambalo alisema sasa kitakuwa kiama cha matapeli wa mtandaoni.

“Nitaliomba Bunge lako mtatusamehe kidogo kwa hili tufumbe macho hata kwenye zile haki za msingi maana kuna mambo yanaudhi, kwa hiyo leo natangaza kiama cha jambo hili.

“Tumejipanga vizuri tutawaomba wenzetu wa polisi na wengine tuondoe huruma kwenye jambo hili tulikomeshe tulifute kwenye nchi yetu,” alisema Nnauye huku akipigiwa makofi na wabunge.

…kupata fedha kirahisi

Katika ripoti iliyopita, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Usimamizi na Maendeleo ya Ujasiriamali, Dk Donath Olomi alizungumzia hali ya ulaghai akisema tatizo jamii ya Watanzania inapenda kupata fedha kirahisi na kwa kuwa hana uelewa wa kutosha wanaishia kuumizwa.

“Watu wanatumia fursa mkato, wakiambiwa ukifanya hivi na hivi unapata fedha basi wanakimbilia haraka, na utapeli huu upo wa aina nyingi kila siku unabadilika na kila siku watu wanalaghaiwa,” amesema Dk Olomi.

Amesema ni muhimu zaidi kuweka nguvu katika uelimishaji wa umma ili kuikinga jamii na ulaghai.

“Miongoni mwa majukumu makuu ya Serikali ni kuwalinda wananchi wake si tu dhidi ya uvamizi bali hata kwa matukio kama haya ambayo yanawarudisha nyuma. Usajili wa laini kwa kutumia vitambulisho vya Taifa tulijua ungemaliza hili lakini mambo bado,” amesema Dk Olomi akihoji mkwamo uko wapi.

Kuhusu kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ulaghai mtandaoni, Mhadhiri msaidizi wa benki na fedha katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Aziz Rashid amesema visa hivyo visipodhibiti vitaathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini pia huenda vikakua na kuathiri uchumi wa nchi.

“Uchumi wa kidijitali miongoni mwa changamoto zake ni ulaghai na uhalifu wa kimtandao. Ulaghai husababisha watu kupoteza pesa, hivyo uchumi wao kuathirika lakini uhalifu wa kimtandao unaweza kutikisha hadi uchumi wa nchi,” anasema Rashid.

Mwalimu huyo wa wanafunzi wa Chuo kikuu cha ARU, anaongeza kuwa ulaghai wa tuma kwa namna hii unapoteza fedha ndogondogo kwa kuwa walio wengi hawatumi fedha nyingi.

Lakaini anasema isipodhibitiwa ikahamia kwenye uhalifu wa kuhamisha mabilioni kutoka benki au kwenye hifadhi ya hiyo mitandao, itakuwa hatari kwa uchumi wa nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live