Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukuzaji wa Uchumi: Tanzania kutumia fursa ndani na nje

Ukuzaji Wa Uchumi: Tanzania Kutumia Fursa Ndani Na Nje.png Ukuzaji wa Uchumi: Tanzania kutumia fursa ndani na nje

Fri, 10 Feb 2023 Chanzo: Dar24

Serikali nchini, inaendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kushirikiana na nchi mbalimbali duniani ili kukuza uchumi wa nchi kupitia fursa za biashara, uwekezaji na utalii zilizopo ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Felista Njau kuhusu umuhimu wa Serikali wa kuainisha nchi zenye fursa za biashara na uwekezaji, ili kukuza pato la Taifa.

Amesema, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na Balozi za Tanzania imeendelea kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zenye manufaa kwa Taifa na kwamba Wizara inaandaa Mpango wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi utakaojumuisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kufikia malengo tarajiwa.

Mpango huo ambao unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba 2023, pia unalenga kuhakikisha fursa za biashara, uwekezaji na utalii zinakuwa na tija zaidi kwa wananchi wa Tanzania na utajumuisha Sekta zote husika ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo muhimu ya kisekta yatakayo changia katika kukuza uchumi na pato la Taifa.

Kuhusu mkakati wa utoaji elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Diplomasia ya Uchumi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali.

Dkt. Tax amefafanua kuwa mpango mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi unaoandaliwa, pia utajumuisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu dhana hiyo, ili kuwawezesha wananchi kuielewa dhana hii na kuwawezesha kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali.

Chanzo: Dar24