Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukusanyaji mapato kielektroniki kutumika kwenye minada ya mifugo

14348 Pic+ukusanyaji TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki katika minada ya mifugo nchini utaongeza mapato maradufu tofauti na ilivyokuwa awali ambapo makusanyo hayo yalikuwa madogo.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Agosti 28, 2018 na katibu tawala msaidizi Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo katika mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa minada nchini, juu ya uendeshaji wa minada na utumiaji wa  mfumo wa kielektroniki.

Mkongo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni moja ya wizara tegemeo nchini lakini changamoto iliyopo ni namna ya uendeshaji na ukusanyaji fedha unavyofanyika katika minada mingi.

Amesema katika minada hiyo unafanyika ukusanyaji uliojaa udanganyifu.

“Ni kweli kumekuwa na ukusanyaji hafifu katika minada na kupoteza fedha za Serikali ambazo zingeweza kusaidia miradi mkubwa inayoendeshwa nchini,” amesema katibu tawala huyo.

Alisema kuingia katika mfumo wa ukusanyaji wa kielektroniki ni wazi kuwa kutakuwa na ongezeko la mapato.

Amewataka wasimamizi hao wa minada watakapoanza kutumia mfumo huo kuhakikisha wanafuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo bila kumuonea wala kumpendelea mtu ili kufikia lengo la Serikali.

Naye mkurugenzi msaidizi wa mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Sopia Mlote amesema ukusanyaji wa maduhuli kwa kutumia njia ya kawaida ulikuwa na matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kuwekwa takwimu zisizo na uhakika.

Amesema kwa njia hiyo ya kisasa, wizara itakuwa ikipata taarifa sahihi za kinachotokea katika minada hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz