Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Ukuaji wa uchumi uwafikie wananchi’

Uchumi Uchumiiii (600 X 300) ‘Ukuaji wa uchumi uwafikie wananchi’

Thu, 20 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Serikali imetakiwa kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo mikoa yote ili ukuaji wa uchumi uwafikie wananchi.

Wito huo umekuja wakati Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) likiwa limetoa ripoti yake inayoonyesha kuwa pato la Tanzania (GDP) limepanda hadi kufikia Dola bilioni 85.42 (Sh199.47Trilioni) katika ripoti yake iliyotoka mwisho wa wiki iliyopita.

Akizungumza jana Aprili 19, kwenye mjadala ulioendeshwa kupitia Mwananchi Twitter Space, ukiwa na mada inayohoji ‘Ukuaji wa pato la Taifa unaendana na uchumi wa Wananchi?’ Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus amesema ongezeko hilo linapaswa kuakisi maisha ya wananchi kwa kupelekewa maendeleo.

“Nadhani tuwe na kasi ya kusudi kuhakikisha miradi hii ya maendeleo inasambazwa hata mikoa inayohitaji uchechemuzi wa kiuchumi hasa maeneo ambayo hakuna viwanda.

“Tuwekeze zaidi kwenye kilimo ili tuweze kuongeza thamani ya mazao wanayozalisha, kwa namna hii tunaongeza mzunguko wa fedha katika maeneo hayo,” amesema Dk Faraja Kristomus

Dk Fraja ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kijamii, amesema hali hiyo itachochea mikoa yote kupanda kwa mapato yake na kupunguza matabaka ya watu yanayoweza kujitokeza siku za usoni.

Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude amesema kukua kwa pato la Taifa kunapaswa kuendana na huduma bora pamoja na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kuthaminishwa kifedha.

“Pato la Taifa inatusaidia, lakini ni jinsi gani uchumi huo unafanya kazi? Kuna uhusiano kati ya ukuaji wa uchumi na pato la mtu mmoja mmoja. Lazima uchumi wa nchi ukue ndipo watu waone manufaa,” amesema.

Chanzo: mwanachidigital