Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukataji tiketi wa treni Tanzania sasa kielektroniki

101347 Pic+tren.png Ukataji tiketi wa treni Tanzania sasa kielektroniki

Tue, 7 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limezindua mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki ikiwa ni mkakati wa kujiimarisha katika utoaji wa huduma na ukusanyaji mapato.

Mfumo huo umezinduliwa leo Jumamosi Aprili 4, 2020 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe amesema TRC imetekeleza agizo la Serikali ya Tanzania kwa kuwa kila shirika la serikali linatakiwa kuwa na mfumo mpya wa malipo wa kielektroniki.

"Nimefurahishwa  sana na hatua hii iliyofikiwa TRC ya kuwa na mfumo wa kukusanya mapato, nina imani shirika  litaimarisha uendeshaji wake ili kupunguza matumizi, kuongeza ufanisi pamoja na kuongeza mapato,” amesema Waziri Kamwelwe

“Serikali imekua ikielekeza TRC kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ili kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wenye tija hasa katika ukusanyaji wa mapato ya kielektroniki” amesema.

Waziri huyo amelipongeza  shirika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao –EGA kutekeleza agizo hilo la serikali na kutengeneza mfumo wa tiketi wa kielektroniki (E-Ticket) na usimamizi wa mizigo kwa njia ya mtandao (E-Cargo) .

Pia Soma

Advertisement

Amesema mfumo wa kielektroniki  utaondoa kabisa matumizi ya tiketi za kuandika kwa mkono.

Kamwelwe amesema kwa mwaka 2017/2018 kabla ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa tiketi, TRC ilikua ikikusanya mapato ya Sh39.7 bilioni na baada ya kuanza kwa matumizi ya mfumo huu mapato yameongezeka na kufikia kiasi cha Sh44.7 bilioni kwa mwaka 2018/2019.

Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwataka TCR kuhakikisha wanaimarisha huduma zao hususan suala la mizigo ya abiria kuwa inapotea na wahusika wanapofika ofisini kutoa taarifa wanapokelewa lakini wanaanza kuzungushwa.

Amesema kuna taarifa alizonazo, baadhi ya wahusika wa mizigo kutokana na umri wao kuwa mkubwa  “wanaamua kuzira” lakini watumishi wa TRC wanafanya mchakato fedha za mzigo ulipotea zinatoka na wanazigawana jambo alilosema hawezi kukubali kuliona likiendelea kutokea.

 

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC, Profesa John Kondoro amesema uzinduzi wa mfumo ni miongoni mwa maagizo aliyotoa Desemba mwaka 2019 ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kukata tiketi ambao hivi sasa umekamilika na umeanza kufanya kazi .

Awali, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mfumo wa Mawasiliano (Tehama) wa TRC, Senzige Kisenge amesema, “ukiwa na kifaa chochote kinachopokea mtandao wa ‘internet’ unatembelea Tovuti TRC utapata maelekezo na utaweza kupata tiketi yako, hatua ni rafiki na rahisi hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wateja wetu.”

Mkurugenzi wa huduma za Tehama kutoka EGA, Benedict Ndomba amesema  EGA ina wajibu wa kuhakikisha matumizi ya Tehama serikalini yanakuwa bora ili kuboresha utoaji huduma  kwa umma.

Chanzo: mwananchi.co.tz