Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukanda huru wa biashara Afrika kuzalisha ajira

Keagan.jpeg Exaud Kigahe akizungumza wakati wa kongamano

Tue, 15 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara,Exaud Kigahe amesema kupitia utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area - AfCFTA), ajira nyingi zitatengenezwa kwenye mnyororo wote wa thamani kuanzia mashambani hadi viwandani.

Mkataba wa AfCFTA ulitiwa saini katika Mkutano wa 10 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika tarehe 21 Machi, 2018 Kigali Rwanda.

Kupitia Bunge, Tanzania iliridhia Mkataba huo tarehe 9 Septemba 2021 na kuwasilisha Hati ya kuridhia tarehe 17 Januari 2022.

Kigahe amesema hayo wakati akifungua Warsha ya Uhamasishaji na Kujenga Uwezo wa Sekta Binafsi katika kutumia fursa za masoko na biashara kupitia utekelezaji wa Mkataba huo. Warsha hiyo iliandaliwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wabia wa maendeleo TMEA na Sekretariati ya AfCFTA jijini Dar es Salaam.

Alisema mbali na ajira, itakuwa ni fursa ya soko kwa watanzania la kuuza bidhaa za viwandani na mashambani, kuvutia uwekezaji na kuongeza mnyororo wa thamani.

"Mkataba huo unatoa fursa ya kuwa na soko la pamoja la bidhaa na huduma lenye jumla ya nchi 55 zenye takriban watu bilioni 1.2.

"Nchi zote 55 za Umoja wa Afrika zina pato la taifa lenye thamani ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4 na fursa za uchumi unaokua kwa kasi," Alisema.

Aliongeza kuwa makubaliano ya mkataba huo yanatarajiwa kuongeza mchango wa biashara wa Afrika kwenye soko la dunia kwa asilimia 2.8 huku sekta za kilimo, chakula na huduma zikipewa nafasi kubwa katika ukuaji huo.

Alisema kutokana na fursa hizo wizara imeona ni vyema kuanzia kuandaa wadau hususan sekta binafsi ili waweze kuchangamkia ipasavyo fursa ya masoko na biashara pindi biashara itakapoanza kufanyika chini ya mkataba huo wa AfCFTA.

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uwepo wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu ili bidhaa zizalishwe kwa gharama ndogo hatimaye zihimili ushindani wa bei na ule wa ubora.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark East Afrika (TMEA) nchini Tanzania, Monica Hangi amesema kuwa wameandaa mkutano huo kujenga uwezo wa sekta binafsi kutumia fursa za kibiashara zilizopo katika eneo huru la Afrika.

Kwa upande wake Dkt. Halima Noor, Mwakilishi kutoka Sekretariet ya AfCFTA, alisema wakati umefika kwa nchi za Afrika kufanya biashara zaidi kwa kutegemeana ili kuwa watoaji wa huduma bora duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live