Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukame wapaisha bei ya nyama Dar

NYAMAS Ukame wapaisha bei ya nyama Dar

Mon, 17 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Bei ya nyama katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam imezidi kupanda na kufika Sh9,000 mpaka Sh10,000 (kulingana na maeneo), kutoka Sh8,000 kwa kilo.

Wakati kitoweo hicho kikipanda, bei ya dagaa ambayo miezi miwili iliyopita ilikuwa imefika Sh12,000 kwa kilo, kwa sasa imeshuka na kuuzwa kati ya Sh7,000 hadi Sh9,000 kwa kilo.

Utafiti uliofanywa kwenye masoko ya Buguruni, Ilala na machinjioni Vingunguti umebaini bei ya nyama ya jumla ni kati ya Sh8,000 hadi Sh8,200, huku ya rejareja ikiuzwa Sh9,000 kwa kilo.

Nyama ya mbuzi nayo imefika Sh12,000 kwa kilo kutoka Sh10,000 iliyokuwa ikiuzwa miezi miwili iliyopita.

Akilizungumzia hilo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika Machinjio ya Vingunguti, Joel Meshack alisema zipo sababu mbili kubwa zilizochangia bei ya bidhaa hizo kupanda, ikiwamo kupungua kwa mifugo inakopatikana kunakochangiwa na hali ya ukame na kufunguliwa soko la nyama nje ya nchi.

“Mfano ng’ombe mwenye kilo 80 hadi 100 aliyekuwa akiuzwa Sh600,000 hivi sasa anauzwa Sh700,000, huku wa kilo 100 hadi 120 aliyekuwa akiuzwa Sh1.2 milioni amefika Sh1.6 milioni,” alisema Meshack. Kuhusu kufunguliwa soko la nje alisema: “Kuna wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanakwenda vijijini kwa wafugaji kununua mifugo, jambo ambalo naona siyo sawa, Serikali iliangalie”.

Kwa upande wa mfanyabiashara wa bucha soko la Buguruni, Sudi Amir alisema kwa sasa sokoni hapo wanauza nyama kilo Sh9,000 kutokana na bidhaa hiyo kupanda bei machinjioni.

Alisema: “Tunakutana na wafanyabiashara kutoka visiwa vya Comoro ambao ng’ombe anayeuzwa kwa Sh1.2 milioni wao hupanda dau na kumnunua kwa Sh2 milioni”.

Naye Meneja wa mnada wa Pugu, Dk Maxmilian Kintu akieleza hali ya upokeaji mifugo ndani ya kipindi cha Agosti na Oktoba, alisema imepungua kutoka ng’ombe 1,000 hadi 1,200 kufikia ng’ombe 700 hadi 800.

Alisema uhaba huo pia unachangiwa na wafugaji kwenda kutafuta mbali malisho, jambo linaloongeza gharama wanapofuatwa hadi kufikishwa machinjioni.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alieleza mikakati ya kukabiliana na uhaba huo wa nyama, akisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh40 bilioni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Alisema kati ya hizo, Sh5 bilioni zitatumika kuanzisha vituo atamizi 240 vya vijana kwa ajili ya unenepeshaji ng’ombe na kutakuwa na atamizi nane nchini.

Chanzo: mwanachidigital