Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Ujuzi tuliopata utaharakisha upanuzi, ukuaji wa uchumi’

710d212e3c80db5cb50ba401fd98ebab ‘Ujuzi tuliopata utaharakisha upanuzi, ukuaji wa uchumi’

Wed, 17 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

“KUHITIMU Programu hii ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program - CAP), ni deni kwa watu ninaowaongoza na jamii nzima ya Watanzania,” anasema Anna Shanalingigwa.

Yeye ni mmoja wa wahitimu 16 wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Jukwaa la Taasisi ya Wakurugenzi na wamiliki wa makampuni binafsi nchini (CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt).

Mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwawezesha watanzania kushika nyadhifa za juu za Uofisa Mtendaji Mkuu (CEOs) na Ukurugenzi Mtendaji (MDs) katika makampuni na taasisi mbalimbali, tayari yamewanufaisha wahitimu watatu akiwamo Anna Shanalingigwa.

Anna ambaye amehitimu Januari mwaka huu, alipandishwa cheo katika kipindi cha mafunzo hayo na kuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Asasi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo (PASS).

Mwanamama huyu anasema ili kufikia malengo hayo ya kushika nyadhifa za juu za Uofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Ukurugenzi Mtendaji (MD), kunahitajika nguvu za ziada.

“Kwa sababu mwanamke hata kama una ufaulu mzuri kiasi gani kwenye masomo, kuna nafasi ya mama na mke ambayo jamii inakutegemea uishikilie,” anasema.

Anasema mwanamke anahitaji mkono kutoka kwa wanaume, wafanyakazi na viongozi wake ili awe kiongozi bora kwa manufaa ya kampuni na jamii kwa ujumla.

Hoja hiyo pia inaungwa mkono na mhitimu mwenzake, Rayson Foya ambaye ni Mkuu wa idara ya uchumi katika benki ya Standard Chartered ambaye anasema mafunzo hayo yatamwezesha kujiamini na kushindana katika nafasi za juu ambazo zimekuwa changamoto kwa Watanzania kuzipata.

Mbali na Anna ambaye amepandishwa cheo baada ya kupata mafunzo hayo, pia Anael Samuel amepandishwa cheo na kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Songas, ilihali Julius Ruwaichi naye akipandishwa cheo na kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Access Bank.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chuo cha Strathmore Business School (SBS), yamefanyika kwa muda wa miezi 12 na kushirikisha makampuni binafsi (CEOrt)

WAZO LA KUANZISHA CAP

Mwenyekiti wa CEOrt, Sanjay Rughani anasema wazo la kuanzisha mafunzo hayo lilitokana na utafiti ambao waliufanya na kubaini kuwa makampuni mengi yangependa kuwa na watendaji wakuu Watanzania lakini wenye sifa ni wachache.

“Baada ya kufanya utafiti ilibainika kuwa asilimia 60 ya viongozi wa kampuni mbalimbali wenyewe walitaka Watanzania na Waafrika wamiliki hizi nafasi za mkurugenzi mtendaji lakini kuwapata hawa Ma-CEOs ilikuwa kazi ngumu sana,” anasema Rughani.

Rughani ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, anasema kabla ya utafiti huo alibaini kuwa benki hiyo yenye umri wa zaidi ya miaka 98, haikuwahi kuongozwa na ofisa mtendaji mkuu kutoka Tanzania.

“Ndipo nilipozungumza na Mwenyekiti wa CEOrt aliyenitangulia, Hayati Ali Mufuruki, tukafanya utafiti huu katika nchi nne na kuja na wazo hili la kuanzisha mafunzo haya hapa nchini.”

Anasema mafunzo hayo pia yamelenga kuwajengea wataalamu wa Kitanzania uwezo mkubwa ili waweze kushindana katika kuhudumu kwenye nafasi za utendaji mkuu katika taasisi, programu na miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa.

“Katika programu hii washiriki 16 ambao wamehitimu, wametoka kwenye kazi zao kama za ofisa rasilimali watu na nyingine lakini watatu kati yao wamepandishwa cheo na kuwa Ma-CEOs katika makampuni ya Songas, PASS na Access Bank.

“Kwa kweli nina furaha kubwa kwani nilikaa tangu siku ya kwanza ya mafunzo na sasa wanaweza kuzungumza mambo ya kidunia, kisera, kiuchumi na kuwezesha kampuni kupiga hatua,” anasema.

WAZIRI MKUU TOA MBINU KUIBUA WATANZANIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye aliwatunuku vyeti wahitimu hao katika mahafali hayo ya kwanza, pia alitoa wito kwa Bodi ya Wakurugenzi ya CEOrt kushirikiana na serikali pamoja na taasisi nyingine ili kubaini maeneo yenye uhitaji wa viongozi wakuu wazawa na kutoa mafunzo yenye tija.

Anasema pia ni vema bodi hiyo ikajipanga kuandaa mipango ya mafunzo yenye lengo la kutambua na kujenga uwezo kwa Watanzania katika sekta za kipaumbele hususani sekta ya madini, mafuta na gesi, ujenzi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Pia Waziri Mkuu anasema ushirikiano wa CEOrt pamoja na Taasisi ya Uongozi inayoendesha programu za mafunzo ya uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Alto cha Nchini Finland, utaleta tija, kuondoa marudio na kuimarisha ubunifu katika kutoa mafunzo na kuleta manufaa kwa washiriki wa mafunzo hayo.

“Huu ni muda mwafaka kwa CEOrt kushirikiana katika kuwajengea uwezo wa wataalamu wabobezi katika masuala ya uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

“Mafunzo haya yamekuja katika wakati mwafaka kwani yanaendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘hapa kazi tu’, pia yamekuja katika kipindi ambacho nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo viongozi hao watumie ujuzi na weledi katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miradi,” anasema.

Chanzo: habarileo.co.tz