Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujio wa makao makuu Dodoma kwaongeza bidhaa bandia

86224 Dodoma+pic Ujio wa makao makuu Dodoma kwaongeza bidhaa bandia

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Tanzania bado inakabiliwa na matumizi ya bidhaa bandia ambazo zipo dukani na maeneo mbalimbali sokoni.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 27, 2019 na Ofisa Mawasiliano na Mahusiano mwandamizi wa Tume ya Ushindani (FCC) Frank Mdimi wakati akizungumza na klabu ya wanafunzi wa shule ya msingi ya Mlezi jijini Dodoma ambao wanapinga matumizi ya bidhaa bandia.

Tume ya ushindani imeanzisha klabu tano za wanafunzi wa shule za msingi jijini Dodoma ambazo zitatoa elimu kwa wanafunzi na jamii kuhusu changamoto ya ununuzi na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora zilizopo katika soko.

Klabu hizo zinatoka shule za msingi Mlezi, Chadulu, Kikuyu, Mlimwa na Martin Luther zote za jijini Dodoma pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wakazi wa jiji baada kuwepo kwa ongezeko la bidhaa kunakotokana na ujio wa makao makuu.

Mdimi amesema tangu kuanzishwa kwa klabu hizo Machi 2019 kumekuwa na mafanikio makubwa yanayoonyesha bado kuna matumizi ya bidhaa bandia sokoni hivyo ni jukumu la kila mmoja kupambana na vita hiyo.

“Wanafunzi wamekuwa wajanja na ndiyo wanatusaidia kubaini vingi ambavyo vimepitwa na wakati na hivi karibuni walikamata bidhaa moja ambayo hatuwezi kuitangaza kwa sasa hadi mamlaka zingine zithibitishe lakini wametusaidia kwa kiasi kikubwa,” amesema Mdimi.

Amesema elimu ya mlaji imekuwa ikisambaa kwa kasi wanapowatumia wanafunzi kuliko ilivyokuwa kwa maeneo ya makundi mengine hivyo wameamua kujikita zaidi shuleni ambako wataongeza idadi ya shule ili ujumbe ufike zaidi.

Kwa mujibu wa Mdimi, wameshafanya mawasiliano na mamlaka zingine ili kuanzisha elimu ya mlaji katika mitaala ya shule za msingi na sekondari ili wajenge jamii yenye uelewa kwa kuanzia ngazi ya chini ya familia mpaka ngazi ya juu kielimu.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mlezi, Anicetus Lyimo amesema klabu hiyo imewasaidia wanafunzi kujua haki na wajibu katika mambo ya mlaji ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na ununuzi na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora zilizopo katika soko.

Lyimo amesema ametoa wito kwa Tume ya Ushindani kutoa elimu zaidi katika shule za vijijini ambako wengi bado wana uelewa mdogo juu ya masuala ya mlaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz