Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujio wa BajajI, Bodaboda ulivyoua biashara ya Taksi Mbeya

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

beya. Kilio cha madereva wa taksi kimezidi kuongeza wakilalamikia biashara kuwaendea kombo.

Ukisikiliza nchi nzima katika miji mikubwa yenye usafiri wa taksi hususani Dar es Salaam, madereva wake wamekuwa wakilalamikia kupungua kwa abiria na kuathiri mapato yao. Sababu kubwa inayotajwa ni kuwepo kwa vyombo vingine vya usafiri vinavyotoa huduma kwa bei ya chini zaidi.

Jiji la Mbeya nalo halikusalimika katika kuyumba kwa biashara ya taksi.

Kutokana na ongezeko la watu katika jiji hilo, usafirishaji umekuwa ni huduma muhimu zaidi.

Kwa sasa karibu kila kona ya jiji hilo inafikika kwa urahisi kutokana na uwepo wa barabara zilizounganika vizuri, kupitika wakati wote na kuwepo kwa aina mbalimbali za usafiri wenye gharama nafuu.

Miaka kadhaa nyuma jiji la Mbeya lilitawaliwa zaidi na usafiri wa daladala na taksi huku barabara nazo zikiwa katika kiwango kisicho cha kuridhisha.

Kipindi hicho usafiri wa taksi ulikuwa maarufu na ukionekana kuwa wa hadhi ya juu na huu ndiyo wakati ambao kwa wananchi wa hali ya chini walitumia mikokoteni kubeba mizigo yao kutoka sehemu moja kwenda nyingine huku taksi zikitumika zaidi usiku kunapokuwa hakuna daladala.

Kuanzia miaka ya 2010 hadi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la usafiri wa pikipiki (bodaboda) na bajaji jambo ambalo limekuwa mkombozi kwa wasafiri huku likuwa ni janga kubwa kwa madereva taksi kwani watu wengi hukimbilia bodaboda au bajaji kutokana na unafuu wa gharama huku zikiweza kumfikisha abiria mpaka maeneo ya vichochoroni ambako pengine taksi isingeweza kufika.

Hivi sasa takribani vituo vyote vya kushusha na kupakia abiria vina aina tatu ya usafiri, bodaboda, bajaji, taksi na daladala, hivyo kumpa uhuru abiria kuchagua usafiri gani autumie kulingana na umuhimu wake kwa wakati huo.

Kutokana na uwepo wa aina zote hizo za usafiri, abiria wengi kwa sasa hususani wenye haraka hupenda kukodi bodaboda na iwapo ana mzigo basi huchukua bajaji ambazo hata gharama zake ni nafuu ukilinganisha na taksi.

Madereva taksi walia

Dereva taksi Ezekia Mwamakamba wa kituo cha daladala Kabwe, anasema kwa kiasi kikubwa ujio wa bajaji na bodaboda umeathiri biashara yao kwa kuwa sasa wanakosa wateja tofauti na ilivyokuwa awali.

“Unaweza kukuta mtu anataka taksi lakini ukimtajia bei na akijua kwa umbali uleule kwa bajaji anakwenda kwa nauli iliyo chini ya uliyomtajia, bila ya kuomba kupunguziwa anaondoka akijua bajaji zipo,” anasema Mwamakamba.

Mwamakamba anasema kwa sasa biashara ya taksi imekuwa ngumu kiasi kwamba inaweza kutokea siku dereva anashinda kijiweni kutwa nzima bila ya kupata hata mteja mmoja.

Anasema “Mambo yamebadilika, hizi bodaboda na bajaji zimeua kabisa biashara ya taksi. Maisha yanazidi kuwa magumu kwani unaweza kushinda siku nzima usipate mteja, japo siku moja moja unaweza kuambulia chochote kitu lakini si kama ilivyokuwa huko nyuma”.

Dereva huyo anasema wateja wao waliowengi kwa sasa ni watu wanaokwenda kwenye kumbi za starehe usiku, wageni wasiolifahamu vyema jiji la Mbeya, wajawazito na waliojifungua kwa njia ya upasuaji ambao hutumia usafiri huo ili kuwahishwa hospitali au kuwarudisha nyumbani kwa usalama zaidi.

Naye dereva taksi wa kituo cha Uhindini, Maison Mwalyanzi anasema amekua akiifanya biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 10, lakini sasa ameona jinsi inavyokuwa ngumu kwa kukosa wateja kutokana na ujio wa bajaji na bodaboda.

“Sasa kama hapa nime-pack (nimeegesha) gari naweza nikalianua jioni bila kupata kitu, na kodi yao iko palepale ambapo natakiwa kulipa Sh150,000 kwa mwaka. Hapo bado bima, fedha ya jiji na ushuru wa maegesho kila siku. Ukipiga hesabu utaona mwenyewe jinsi biashara hii ilivyo ngumu. Kwa kifupi biashara hii kwa sasa imekuwa ya kubahatisha,” anasema Mwalyanzi.

Mwalyanzi anasema kwamba anashindwa kuacha kazi hiyo kwa sababu ndiyo aliyoizoea japo amewahi kufikiria kuachana nayo na kuamua kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kurudisha leseni.

Mwalyanzi anasema ingekuwa afadhali kama tozo kwa magari hayo itapungua na kuwa kama ilivyo kwa bajaji ikiwamo kuweka mipaka ya kutoa huduma ili waweze kugawana wateja.

Dereva mwingine, Alphonce Mwakyandali anasema mbali na ujio wa bajaji na bodaboda kuchangia kutikisa soko la taksi, kutikisika kwa hali ya kipato kwa wananchi wengi nako kumechangia kubadilika kwa mfumo wa matumizi ya familia ikiwamo matumizi ya vyombo vya usafiri.

Anasema: “Zamani ilikuwa raha sana kwani unaweza kupata mteja anakodi taksi anataka umpeleke Kyela, Mbarali au Tunduma na gharama yake ilikuwa haipungui Sh300,000, wakati mafuta unayotumia labda ni ya Sh70,000 tu, hivyo unabakiwa na salio la kutosha”.

Hali ikoje maeneo mengine

Kilio cha bajaji na bodaboda kuua soko la taksi hakipo Mbeya tu, kwani hivi karibuni umewahi kushuhudiwa mgogoro kati ya bajaji na taksi katika miji ya Moshi na Morogoro.

Kote huko kilio kikubwa kinaanzia kwa madereva taksi au daladala wanaoshinikiza bajaji ziwekewe mipaka katika kuchukua abiria ikiwa ni dalili kwamba hali ya biashara kwao imekuwa ngumu.

Mjini Moshi mwishoni mwa mwaka jana madereva wa daladala waligoma kutoa huduma kwa siku tatu wakishinikiza bajaji zisiruhusiwe kuingia katikati ya mji hususani katika vituo vya daladala kupakia abiria. Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia mkoani Morogoro ambako madereva wa daladala waligoma kutoa huduma wakishinikiza bajaji zisifike mjini.

Bila shaka ujio wa bajaji, bodaboda na hata kampuni nyingine zinazotoa huduma ya usafiri kwa gharama nafuu zitaendelea kuziumiza taksi kama nazo hazitabuni namna ya kuweza kuhimili ushindani.



Chanzo: mwananchi.co.tz