Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salaam- Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 umekamilika kwa asilimia 70.
Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 7, 2020 wakati akiahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 mjini Dodoma.
Amesema ujenzi kwa sehemu ya Morogoro – Makutupora (kilometa 422) unaendelea.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuendelea na ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere ambako kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa daraja la muda, utafiti wa miamba na udongo na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini wenye urefu wa mita 147.6.
Amebainisha kuwa Serikali imefanikiwa kuendeleza mradi wa umeme vijijini (REA), kwamba hadi Desemba 2019 vijiji 8,236 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishwa na umeme, sawa na asilimia 67.1.
Pia Soma
- Serikali ya Tanzania yatumia Sh128 bilioni kuboresha elimu ya msingi
- Uraia wenye mashaka wanyima vitambulisho maelfu ya wananchi Geita
- Bunge la Tanzania laridhia azimio la kufuta madeni
Kuhusu usafiri wa anga, Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11.
“Hadi Desemba 2019, ndege nane zimepokelewa na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu yameshafanyika.”
“Kuzinduliwa kwa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na kuanza kutumika kuhudumia abiria, kuendelea na uboreshaji wa kiwanja cha ndege Mwanza na viwanja vya mikoa mbalimbali,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya.