Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tano kinachoanzia Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga umefikia asilimia 28.
Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC) waliotembelea mradi huo eneo la Fella Wilaya ya Misungwi jana Machi 28, 2023, Meneja wa mradi huo, Christopher Kalisti ameahidi kuwa mradi huo utakamilika ndani ya muda kulingana na mkataba.
Kwa mujibu wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa Kilometa 342 unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh3.06 trilioni unatakiwa kukamilika Mei, 2024.
“Serikali inatekeleza mahitaji muhimu ikiwemo malipo ya fedha ambapo hadi kufikia Februari 28 mwaka huu, mkandarasi alikuwa ameshalipwa zaidi ya Sh700 bilioni,” amesema Kalisti
“Hadi sasa, tayari mataruma ya reli imetandazwa katika eneo lenye urefu wa Kilometa nne; na kwa kasi hii, tunaamini mradi huu utakamilika Mei, 2024 kwa mujibu wa mkataba,” amesema
Kuhusu huduma kwa wafanyakazi, Meneja mradi huyo amesema uongozi unatoa huduma bora za msingi ikiwemo chakula, malazi na usalama kazini, lengo likiwa ni kuongeza ari ya kazi kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kikamilifu ili kukamilisha mradi kwa wakati.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa PIC, Jerry Silaa amesema Kamati yake imeridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa mradi huo huku akiwataka wananchi wanaoishi maeneo jirani kutumia fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi kupitia biashara na huduma kwa wafanyakazi wa mradi.
“Kwa taarifa hizi na kwa kujionea wenyewe, tunawatoa hofu hofu wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huu kwa sababu Serikali inatimiza wajibu kwa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati kulingana na thamani halisi ya fedha za umma zinazotumika,” amesema Silaa
Mwenyekiti huyo kupitia kamati yake ameuagiza uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na mamlaka zote za Serikali zinazohusika kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili siyo tu ukamilike kwa wakati, bali pia kwa ubora unaolingana na thamani halisi ya fedha.
"Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam na maeneo kwa muda mfupi. Wataalama wametueleza kuwa wanaotoka Mwanza asubuhi wataweza kula chakula cha mchana Dar es Salaam. Haya ni mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini," amesema Silaa
Diwani wa Kata ya Mkuyuni jijini Mwanza, Donatha Gapi amesema kukamilika kwa mradi huo siyo tu utaboresha na kurahisisha sekta ya usafirishaji, bali pia utakuza uchumi na pato la wananchi na Taifa kwa ujumla kupitia fursa ya uwekezaji, biashara na ajira, hasa kwa vijana.