Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi kiwanda cha mbolea wafikia 65%

Caa0616de0dea9c80071a29ebab66706 Ujenzi kiwanda cha mbolea wafikia 65%

Wed, 2 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ujenzi wa kiwanda cha mbolea chenye uwezo wa kuzalisha tani 6,000 kwa mwaka, umefikia asilimia 65 na kinatarajiwa kuanza kazi Julai mwaka huu.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alitoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (NRFA) alipotembelea ofisi za mamlaka hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara ya mbolea ya kimataifa.

Mavunde alisema kiwanda hicho cha mkoani Dodoma kikikamilika kitapunguza gharama ya mbolea nchini ambayo imekuwa ikiuzwa kwa gharama kubwa kutokana na asili ya uzalishwaji wake na kuwa asilimia kubwa inaagizwa kutoka nje ya nchi.

“Serikali inatambua nafasi kubwa ya sekta ya mbolea katika kuchagiza maendeleo ya kilimo nchini, hakika kilimo kinategemea mbolea na kwa kuwa na kiwanda chetu nchini itakuwa na uhakika wa kuwa na mbolea na tena itauzwa kwa bei ya chini,” alisema Mavunde.

Mavunde alizungumzia kuhusiana na maendeleo ya ujenzi wa maabara ya kisasa inayojengwa na NRFA. Mbali na kupongeza utendaji kazi wa mamlaka hiyo, ameitaka kufanya ununuzi wa vifaa vyote vya ujenzi vinavyotakiwa mapema ili kumwezesha mkandarasi kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Alisema ujenzi wa maabara hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais na ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuboresha mazingira ya kusimamia na kudhibiti ubora wa mbolea nchini.

Akizungumzia manufaa ya maabara hiyo, Mavunde alisema itawasaidia wadau wa mbolea katika kupata majibu ya uchambuzi kwa wakati.

Aidha, itapunguza gharama ya mbolea kutokana na bei ya bidhaa hiyo kuongezeka kutokana na kucheleweshwa kwa majibu ya uchambuzi yaliyokuwa yakifanywa na vyombo binafsi na hivyo kuongeza gharama ya kutunza mzigo huo bandarini.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephan Ngailo alisema maabara hiyo yenye viwango vya kimataifa ikikamilika itakuwa maabara pekee Afrika Mashariki na Kati katika upimaji wa sampuli za mbolea.

Alisema serikali itahakikisha maabara hiyo inapata ithibati ya kimataifa ili uchambuzi wake ukubalike duniani kote na mbolea inayopimwa katika maabara hiyo itambulike kwa ubora wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live