Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imeelezwa kuwa ujenzi wa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze, umefikia umefikia asilimia 59 na ule wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umefikia asilimia 92.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 17, 2023 mjini Chalinze na Meneja mradi wa kituo hicho, Mhandisi Newton Livingstone baada ya kamati hiyo kutembelea na kukagua maendeleo yake.
Amesema mradi huo unajumuisha miradi mikubwa miwili ambayo ni pamoja na wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa kutoka JNHPP hadi kituo cha Chalinze kwa msingi wa kilovoto 400 yenye urefu wa kilomita 160 ambao wenye thamani ya Sh51.5 milioni na Sh39.12 bilioni pamoja na kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze wenye thamani Sh30.85 bilioni, kitakachohusisha ufungaji wa mashine umba sita zenye uwezo wa Megavoti 250 kila moja.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dustan Kitandula amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Nishati kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati miradi hiyo mikubwa.
Amesema kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi kwa kuwa inakwenda kusaidia kwenye sekta ya uwekezaji mkubwa na kukuza uchumi wa nchi.
"Uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi sana sambamba na mahitaji ya upatikanaji wa umeme hivyo, Tanesco hakikisheni mnaweka msukumo mkubwa kwenye miradi hii," amesema Kitandula.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema kukamilika kwa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100, utanufaisha mikoa mbalimbali kwa kuongeza hali ya ubora na uhakika wa upatikanaji wa umeme wa uhakika utakaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Aidha, Byabato ameishukuru Serikali kwa kuidhinisha fedha za kugharamia ujenzi wake ambayo awali, mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze ulikuwa ufadhiliwe na mradi wa North Grid, kabla ya Serikali kuamua kuanza kuufadhili kwa asilimia 100.