Waziri MKuu Kassim Majaliwa ameshuhudia uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Kibiashara cha Afrika Mashariki (EAC) unaofanyika katika eneo la Ubungo, mradi utakao kuwa na maduka 2,060 na kutoa huduma zote za kibiashara ikiwemo benki, ufungishaji na usafirishaji.
Mradi huo ulioko katika eneo la ukuwa wa mita za mraba 75,000 ambalo awali lilikuwa likitumika kama kituo cha mabasi unatekelezwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center ya nchini China kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 500.
Waziri Mkuu amesema mradi huo utazalisha ajira za moja kwa moja zaidi 15,000 na utahamasisha maendeleo ya setka mbalimbali ambazo nazo zitazalisha ajira zisizo za moja kwa moja 50,000 hivyo kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wa Tanzania.
Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2022, Uchumi wa Taifa ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2021
“Ukuaji chanya wa uchumi ni fursa bora kwa wawekezaji na katika hili ninampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake makini wenye lengo la kuliletea taifa letu maendeleo ya haraka-Waziri Mkuu,” amesema Waziri Mkuu.