Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi hoteli wabadili sura

VERDE Ujenzi hoteli wabadili sura

Fri, 10 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI ya Zanzibar imesema kukamilika kwa ujenzi wa Hoteli ya Mkoani Pemba kutabadilisha mazingira ya wilaya hiyo na kuwa kivutio cha wageni kama zilivyo wilaya zingine.

Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa, aliyaeleza hayo juzi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa hoteli hiyo.

“Sasa hali iliyofikiwa haitoshi tena kubakia kama ilivyokuwa zamani, ndiyo maana serikali ikatoa uamuzi mzuri hoteli ya Wete kupewa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), hoteli ya Mkoani kupewa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kuifanyia matengenezo na zimebadilisha mazingira na sote tunaona,” alisema.

Alisema sasa hoteli ina vyumba 18 vya kulala wageni na itasaidia kuongeza mapato ya serikali.Hata hivyo, alipendekeza hoteli hiyo na ukumbi wa Umoja ni Nguvu, kufunguliwa kabla ya serikali ya awamu ya saba haijaondoka madarakani.

Alisema wakati umefika kwa miradi ya ZSSF kuwa ya maendeleo itakayokuwa na tija kwa nchi na wanachama.Pia Balozi Ramia aliutaka uongozi wa ZSSF kuhakikisha hoteli hiyo inaendeshwa kibiashara na si kutoa huduma, kwa kuwa wanategemea kukusanya kodi kisheria, hivyo lazima wageni walipe watakaohitaji huduma hotelini hapo.

Kuhusu mikakati ya ujenzi wa kiwanda cha mwani Chamanangwe, Balozi Ramia alisema serikali imedhamiria zao la mwani na karafuu kufanywa kuwa mazao makubwa ya nchi.Alisema katika kutilia mkazo hilo, serikali imepandisha bei zao la mwani kutoka Sh. 600 hadi 1,800 kwa kilo huku karafuu bei ikiendelea kama ilivyo sasa.

Kwa upande wa jengo la ofisi za ZRB Pemba, Balozi Ramia alisema azma ya serikali kila ofisi kuwa na majengo ya kisasa ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Joseph Abdalla Meza, alisema mikakati kwa sasa ni kujenga ofisi kila mkoa ili kuwaondolea usumbufu walipakodi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live