Ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi (Daraja la Magufuli) katika ziwa Victoria mkoani Mwanza linalotarajiwa kutumika kuwaonganisha wananchi wa mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Kigoma, Kagera na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi umefikia asilimia 72 kukamilika.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya, amebainisha hilo wakati alipotembelea ujenzi wa Daraja hilo lenye urefu wa Km 3, utakao rahisisha shughuli za wananchi ambao kwa sasa wanatumia kivuko ambacho kinachukua kati ya saa moja hadi mbili huku akieleza kuwa hadi mradi huo utakapokamilika utagharimu takribani bilioni 716.
Kasekenya amesema kwa mujibu wa taarifa za wakandarasi na msimamizi wa mradi utakamilika Februari 2024, na fedha inayotumika katika mradi huo ni ya Tanzania, na hakuna deni ambalo mkandarasi anaidai Serikali, mradi usisimame kwa namna yoyote kwasababu ya kukosa malipo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya ameshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Segerema – Nyehunge (km 54.4) kwa kiwango cha Lami, ambao ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Mwanza hususani katika wilaya ya Sengerema kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.