Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi Bandari ya Malindi, mji wa Bwawani waiva

Bea49d0a1c28b8b6ab4908b4e52a8b1b.PNG Ujenzi Bandari ya Malindi, mji wa Bwawani waiva

Fri, 21 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameshuhudia utiaji saini mpango mkuu na kufanya utafi ti na upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Malindi ambayo itakuwa ya kitalii pamoja na mji wa kisasa katika eneo Bwawani mjini Unguja.

Utiaji saini huo ulifanyika Ikulu jana kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ambayo ni taasisi ya serikali ya nchi hiyo. Aliyetia saini kwa upande wa SMZ ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Amour Hamil Bakari na kwa upande wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ni Shehe Nasser Al Harthy.

Pia Mkurugenzi wa Shirika la Bandari, Nahaat Mahfoudh naye aliweka saini kwa upande wa wizara hiyo na Mohamed Al Taooq alisaini kwa niaba ya mamlaka hiyo ya Oman.

Akizungumza baada ya utiaji wa saini huo, Rais Mwinyi alieleza kwamba katika mradi huo bandari mpya ya Malindi ambayo inatarajiwa kujengwa baada ya kujengwa bandari ya mpya ya makontena Mangapwani, itageuzwa kuwa bandari ya kitalii pamoja na kulitengeneza eneo lote kutoka bandarini Malindi hadi Hoteli ya Bwawani ili eneo hilo liwe na majengo mapya ya burudani, hoteli na majengo ya kuishi.

Alisema eneo hilo ambalo litakuwa la mji mpya wa kitalii linakisiwa kuwa na ukubwa wa hekta 30 ambazo zitatokana baada ya kufukia bahari katika eneo hilo ambalo litakuwa la mji mpya wa kitalii.

Alieleza amefurahishwa kutokana na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kutafuta wawekezaji katika maeneo mbalimbali, Serikali ya Oman mbali ya kutiliana saini na SMZ juu ya ujenzi wa Bandari ya Makontena jana imetiliana saini tena na serikali katika ujenzi huo utakaowezesha kuwa na mji mpya wa kisasa Malindi.

Rais Mwinyi alitoa shukrani kwa kujitokeza kwa wawekezaji hao na kusema kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 zitatumika katika ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.

Aliwapongeza wawekezaji hao waliokuwa na nia ya kuwekeza Zanzibar, akisema Zanzibar inaendelea kutafuta wawekezaji katika maeneo mbalimbali, kwani lengo ni Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar wa Miaka Mitano unatakiwa kushirikisha sekta binafsi kusaidiana serikali kujenga miradi ya maendeleo yenye tija na ile ya kibiashara.

Alisema serikali itaendeleza jukumu lake la kuweka mazingira mazuri pamoja na kuwavutia wawekezaji, ambako kwa yale mambo ambayo wawekezaji hawatoweza kuingia, yatafanywa na serikali kama vile ujenzi wa barabara.

Aidha, alieleza kwamba wawekezaji hao kutoka Serikali ya Oman wana moyo mkubwa hiyo ni kutokana na kuweka fedha nyingi katika mradi huo. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali alisema ujenzi wa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuiletea mendeleo endelevu Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman, Shehe Mohamed Al Taooqi alimhakikishia Rais Mwinyi kwamba watahakikisha mradi huo unafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Awali, Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ilimuonesha Rais Mwinyi michoro na ramani za mradi huo ambao utakuwa wa aina yake na utainua uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Januari 18, mwaka jana, Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ilitiliana saini na SMZ juu ya ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ambayo itajumuisha bandari tofauti ikiwemo ya makontena na mizigo mchanganyiko kazi ambayo hivi sasa inakwenda vizuri na iko katika hatua ya upembuzi yakinifu na hatimaye itaingia katika utekelezaji wa ujenzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live