Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhaba wa pombe unavyotishia ajira, mapato Zanzibar

Bia Pombe Alcohol Scaled Uhaba wa pombe unavyotishia ajira, mapato Zanzibar

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sakata la uhaba wa pombe limeendelea kutikisa visiwani hapa huku wafanyabiashara, wahudumu na wateja wakielezea athari zinazowakumba kutokana na kadhia hiyo.

Sakata hilo lilianza kuibuliwa na Simai Mohammed Said, aliyekuwa waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, mwanzoni mwa wiki iliyopita alipokutana na wadau wa utalii kuzungumzia tatizo hilo, akieleza jinsi sekta ya utalii inayobeba uchumi wa Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 30, inavyoanza kuathirika kutokana na uhaba wa vileo kwenye hoteli.

Simai alisema kadhia hiyo inatokana na alichodai ni kwa sababu ya mabadiliko ya mawakala wa kuingiza pombe, akiituhumu Bodi ya Vileo Zanzibar kubadilisha mawakala na kuweka wapya bila hata kushirikisha wizara, ambayo ndiyo yenye dhamana ya utalii.

“Tumeona maamuzi ya Bodi ya Vileo Zanzibar imewaondosha wale waliokuwa wanahusika kama ZMMI, Schoch na One Stop, nimeanza kuona athari, hoteli nyingi zimeanza kukosa huduma baada ya Bodi ya Vileo kufanya uamuzi huo, niwaombe wawekezaji, waendelee kuwa wavumilivu wakati huu ikitazamwa namna ya kutatua jambo hili,” alisema Simai.

Siku moja baada ya kutoa kauli hiyo, Simai alitangaza kujiuzulu nafasi yake kupitia video ambayo ilisambazwa mitandao na baadaye Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi akaridhia mwanasiasa huyo kujiuzulu ya uwaziri.

Januari 27, mwaka huu, Rais Mwinyi alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mapinduzi na nafasi ya Simai ikajazwa na Mudrick Ramadhan Soraga aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, huku wizara hiyo ikibaki bila kuwa na waziri.

Wafanyabiashara, wahudumu walalama Mwananchi imejiridhidha kuwa kuhusu uhaba wa vileo visiwani hapa, kwenye mahoteli na maeneo mengine mbalimbali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wafanyabiashara, wahudumu na watumiaji wa pombe, wameeleza kuwapo hali hiyo, hususan bia, huku zake zikipanda.

Mfanyabiashara wa vileo, Peter John Sige, amesema wamekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa pombe hasa bia kwa kipindi cha takribani wiki mbili sasa, jambo linalosabaisha bei kupanda.

“Hakuna vinywaji, japokuwa sina uhakika zaidi, lakini kuna mabadiliko ya mawakala kwa sababu ya udhibiti, wanabadilisha mawakala kwa hiyo inaweza kuwa kipindi cha mpito, baadaye hali ikakaa sawa,” alisema.

Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara ya vileo eneo la Amani, Frank John Kahamu amesema vileo ni shida na vimekuwa adimu, na hiyo imeathiri biashara hiyo.

“Hili linaathiri sana watu wengi kwa sababu eneo kama hili wanaingia watu wengi na limeajiri watu wengi sana, kwa hiyo linapokosa huduma kama hii inakuwa shida,” amesema.

Kwa mujibu wa katibu huyo, eneo la Amani pekee kuna watu zaidi ya 3,000 ambao wanalitegemea, ama kwa kujiajiri au kuajiriwa.

“Kiufupi imekuwa vigumu sana na inalazimisha watu wengine kupunguzwa kazini kwa sababu hakuna kazi inayoendelea. Shida kubwa ya hili, kampuni za zamani zimeondolewa na zimeingizwa nyingine mpya,” amesema.

Amesema, “kwa hiyo kampuni hizi mpaka zianze taratibu za kujipanga kuleta mzigo inakuwa changamoto kubwa, inawezekana baadaye hali ikakaa sawa, lakini itakuwa imeathiri biashara kwa kiasi kikubwa.”

Hata hivyo, ameshauri unapofanyika utaratibu wa kubadilisha mawakala isiwe kwa ghafla, watu wapewe muda wa kujipanga kwa kuwa wanaoondolewa wanakuwa tayari wapo kwenye mfumo.

Mmoja wa wahudumu wa baa, Omaira Saad Rashid amesema wanakutana na changamoto kwa kuwa baadhi ya wateja wakiambia kwa kuwa bei zimepanda, wanadhani wanataka kuwaibia.

Omaira amesema pia imepunguza kipato kwao kwani wateja wanapunguza kiwango cha unywaji, akitoa mfano kama mteja alipanga kunywa bia nyingi anapunguza idadi au wakati mwingine anaacha.

Alisema jambo hilo limefanya baadhi ya wahudumu kuachishwa kazi kwa kuwa wanaopata huduma hiyo wamepungua.

Kuna bia zilikuwa zinauzwa Sh2,500 zimepanda bei mpaka Sh3,500, nyingine zimepanda kutoka Sh3,000 mpaka Sh3,500 hadi Sh4,000 kutokana na ujazo na aina ya bia.

“Kwa hiyo imekuwa changamoto, hata ukimwambia mteja bia ni Sh3,500 anadhani kwamba hiyo Sh500 unataka kuichukua wewe, mpaka meneja amweleweshe ndipo anaamini,” amesema.

Mfanyabaishara mwingine wa bidhaa hiyo, Grace Emmanuel amesema chagamoto ni ukosefu wa vinywaji kwani mzigo unaoingia unakuwa mdogo.

“Huu ni mji wa kitalii, bila pombe mambo hayaendi kwa hiyo tunapata shida, watu wanataka kulipwa kodi zao, unajiuliza utalipaje kama hakuna biashara,” amesema.

“Tunapata shida kama mtu hujafanya biashara utalipa nini, kwa hiyo hii inakuwa changamoto ya moja kwa moja, ombi letu Serikali iliangalie jambo hili kwa mapana zaidi kwa faida ya pande zote mbili kwa sababu wapo watu wanaoteseka kutokana na kadhia hii ya kukosa vinywaji,” amesema.

Baadhi ya watumiaji wa vileo walieleza kukumbana na kadhia hiyo inayowafanya kutoenda kustarehe, huku wakiishauri Serikali kama imeruhusu vileo hivyo isiweke vikwazo bali isimamie sheria.

“Kweli bia zimepanda bei, kama kuna sheria na watu wanaouza wamepewa vibali, bora wasimamie sheria hizo kuliko kukosa huduma hiyo,” amesema bila kutaka jina lake kutajwa.

Mwingine amesema licha ya bia kupanda bei, hata mnywaji akiwa na fedha wakati mwingine anaweza kukosa kinywaji anachokitaka.

“Wakati mwingine unaweza kwenda baa ukawa na hiyo Sh4,000 mfukoni, lakini bia huzipati, hili hakika halijakaa sawa katika huduma,” amesema mtumiaji mwingine wa vileo.

Pombe hazipelekwi Zanzibar kwa meli Akizungumzia upatikanaji wa vileo, mfanyabiahara mwingine wa vileo, Jackson Peter amesema kumekuwa na uhaba mkubwa kutokana na vileo kutoingia kama ilivyozoelekea.

Alisema kinachopatikana kwa sasa, japokuwa si kwa wingi, ni pombe kali. “Watu hawafahamu, biashara hii ya pombe, haisafirishwi kwenye meli kama bidhaa nyingine isipokuwa unatakiwa uwe na majahazi yako maalumu kutoka Dar es Salaam na magari ya kusambaza baada ya mzigo kufika bandari ya Malindi,’’ amesema.

Mfanyabiashara mwingine ambaye hakupenda jina lake litajwe amesema anamiliki baa zaidi ya tatu, katika maeneo mbalimbali Zanzibar, na hali wanayokutana nayo sasa haijawahi kutokea kwa miaka mingi tangu aanze biashara hiyo.

“Kama watu wanapewa vibali vya uingizaji wa pombe na hawana majahazi yao, hawana magari ya kusambaza, unategemea nini kama si hiki kinachotokea sasa?  Wanapaswa walitazame hili maana Serikali inakosa kodi kubwa,” afafanua.

Hata hivyo, moja ya maeneo ambayo kwa sasa yanaonekana kukimbiliwa na wanaohitaji huduma hiyo ni jeshini.

Akiendelea kufafanua zaidi kuwa hivi sasa kuna eneo maalumu la Mtoni, wanakokwenda kununua vinywaji kwa jumla nako pia hazipatikani kwa kiwango ambacho mteja anahitaji.

Akitoa mfano, amesema kwa sasa wananunua kreti moja ya bia ya Serengeti kwa Sh41,000 wakati awali walikuwa Sh37,000, hivyo nao wamepandisha bei zaidi.

Amesema wanalazimika kuuza bia moja hadi Sh4,000 kutoka Sh2,500 kwa sababu hawana uhakika kuwa siku inayofuata wanaweza kupata mzigo mwingine.

Mwananchi lilifika kwenye baadhi ya baa maarufu na kushuhudia idadi ndogo ya wateja, tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma kutokana na umaarufu wa baadhi ya baa hizo.

Uchunguzi wa kina umebaini watu wengi wameacha kwenda kwenye maeneo ya uraiani kupata vinywaji, badala yake wamekimbilia kwenye maeneo ya jeshi ambako huko bia zinauzwa bei ya kawaida kuliko ya mtaani iliyopanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live