Taasisi za Kibenki na kampuni zingine zinazojihusisha na uzalishaji wa vinywaji nchini zimeshauriwa kuja na mkakati wa kukabilina na changamoto za maji zinazosababishwa na mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa sekta ya viwanda haiwezi kuwa na tija kiuchumi pasipo kuwa na maji ya Kutosha.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira kutoka Takribani nchi Tano za Afrika, Mkurugenzi wa shirika la Kimataifa la uhifadhi wa mazingira na wanyama pori WWF Aman Ngusaru amesema licha ya serikali kufanya jitihada za kuhakikisha uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji vinapewa kipaumbele sasa ni wakatiwa sekta binafsi zikiwemo kampuni na taasisi za kifedha kuunga mkono jitihada hizo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa TBL Jose Morani amesema kuwa kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) AB InBev wakishirikiana na Shirika la Wanyama Pori Afrika WWF Africa wameamua kuendesha semina ya maji yenye lengo la kuboresha ubora na upatikanaji wa maji salama maeneo yanayo sadikika kuwa katika hatari ya kukosa maji kwa mwaka 2025.
Moran ameongeza kuwa Viongozi kutoka AB InBev na WWF watashirkiana katika miradi endelevu iliyo katika awamu mbali mbali za utekelezaji nchini Tanzania, Uganda, Zambia, na Msumbiji, Mradi wa Usalama wa maji jijini Dar Es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kuongezewa katika ushirika huu, unalenga kuboresha na kuongeza upatikanaji wa maji salama pamoja na kulinda viumbe hai wanaotegemea maji jijini Dar es salaam na miji ya karibu kupitia njia tofauti za ufumbuzi, hasa kwa mto Msimbazi, Mzinga, na Ruvu.
Aidha wamebainisha kuwa Tanzania ina vyanzo vya maji vingi sana ikijumuisha mito, ziwa na ardhi nyevu, lakini jamii nyingi bado hazina upatikanaji wa maji salama ya kunywa, Upatikanaji na usambazaji wa maji salama kwa bei nafuu ni moja wapo ya mipango ya maendeleo endelevu, na ndio lengo kubwa la kushirikiana na shirika la WWF pamoja na wadau nchini Tanzania ili kuweza kushirikiana kuleta matokeo chanya.