Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhaba wa fedha unavyokwamisha ukuaji wa biashara za lishe

Eb34ea9a4339f50db537d70c452979d9 Uhaba wa fedha unavyokwamisha ukuaji wa biashara za lishe

Tue, 13 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la wajasiliamali wahitimu kutoka chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUGECO) ni wahusika wakuu katika mnyororo wa thamani wa biashara ya kilimo na mazao yake.

Shirika hilo lilianzishwa mwaka 2011 kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kilimo na kukuza biashara ya lishe mkoani humo.

Wanaushirika hao wanafanya kazi kimkakati na chuo hicho kikuu cha kilimo ili kukuza mazingira ya biashara ya kilimo katika mkoa huo, wakiwezeshwa na kampuni za uzalishaji wa bidhaa za chakula kama vile Sanavita na Kinshaga.

Kampuni hizo zimekuwa sehemu ya kuhamasisha lishe, programu iliyoanzishwa na kampuni ya Sahara Ventures na Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) nchini.

Sugeco pia inafanya kazi kama kituo cha ukuzaji wa bidhaa na uhamishaji wa teknolojia, ikitoa huduma za maendeleo ya biashara kwa wajasriamali wadogo (SMEs), na mshauri kwa mashirika ya binafsi na ya umma juu ya masuala yanayohusiana na lishe na biashara ya kilimo.

Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na kampuni ya Sahara na Gain Alliance Tanzania, juu ya hali ya biashara ndogo ya lishe kwa wajasiriamali wadogo na wa kati imebaini kuwa mfumo wa ikolojia wa mkoa huo unakua, na hiyo ni kutokana na jitihada zilizofanywa na Chuo Kikuu cha SUA na Sugeco.

Aidha, ripoti hiyo inabainisha bado kuna changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo tatizo la ukosefu wa upatikanaji wa vifaa vya ufungaji vya hali ya juu na vya kuvutia, upatikanaji wa fedha, mashine za kupima yaliyomo kwenye lishe, na masoko mapya ya bidhaa za lishe.

“Sugeco wana jukumu muhimu katika mfumo wa ikolojia wa mkoa, na wanashughulikia masuala mazito kama vile utapiamlo, kumaliza upoteaji wa mavuno, kudhibiti njaa, na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana kupitia biashara ya kilimo," Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike anaeleza.

Pia, anatoa motisha kwa wakulima kujihusisha na kilimo cha Viazi vitamu (OFSP), vinavyojulikana pia kama Viazi Lishe, kwa kuunda mnyororo wa thamani ya biashara kwa kuwaunganisha wakulima na wauzaji wa chakula wa ndani pia wanaojulikana kama Mama Lishe na Baba Lishe.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waanzilishi hao wa biashara wamekuwa wakifanyakazi na wafanyabiashara wa chakula katika maeneo ya Dumila na Manispaa ya Kilosa na wamekuwa wakiwasaidia wanawake na vijana katika kuzalisha na kutengeneza na kuongezea thamani OFSP.

“SUGECO pia wamekuwa wakifanyakazi na wajasiriamali wakiwasaidia kujifunza kutengeneza mkate wenye afya zaidi kwa kutumia viazi lishe badala ya ngano. Waanzishi hao wa biashara wanawasaidia wajasiriamali kutengeneza mahitaji kutoka shule za msingi na sekondari ili zichukue mkate wa OFSP badala ya mkate wa ngano, "Mtambalike anasema.

Aidha, bidhaa nyingine zinazozalishwa kupitia waanzishili hao wa biashara kutoa SUA ni biskuti za ndizi zilizopewa jina la Akili kutoka kampuni ya Kinshaga, unga wa Sanavita wa viazi lishe kutoka Sanavita na biskuti za viazi lishe kutoka kampuni ya SolarTunda.

“Jambo tulilojifunza kupitia Sugeco pamoja na kwamba wajasiriamali wanafanyakazi kwa juhudi kuzalisha bidhaa za chakula zenye lishe na afya, bado wanakabiliwa na changamoto ya kuzalisha bidhaa zenye viwango vinavyokubalika katika masoko ya kimataifa,” anasema Mtambalike.

Mwanzilishi wa kampuni ya Kinshaga, Elias Kinshaga anaelezea wasiwasi na matatizo aliyoyapata wakati akianzisha kampuni yake hiyo kuanzia chini hadi hapo ilipofikia ikiwemo uzoefu wake katika kukabiliana na taasisi za fedha wakati akitafuta mtaji.

Mfanyabiashara huyo anaeleza wazi kuwa kupata mkopo kutoka kwenye benki za ndani kuna changamoto na hatua nyingi zinazohitaji kazi kubwa.

“Benki za ndani nyingi hazina uelewa wala huduma za mikopo kwa wajasiriamali wadogo na huwachukulia wajasiriamali hao kama wachanga wa biashara,” anaeleza Kinshaga.

Kampuni hiyo hatimaye ilipata fedha na kupata mtaji lakini kwa bahati mbaya kutokana na kuibuka kwa virusi vya corona, ilikabiliwa na ucheleweshaji wa uzalishaji kwa sababu ya ugumu wa kupokea mashine wanazohitaji kwa uzalishaji iliyokwama nchini China.

“Benki zimekuwa zikitaka biashara ziendelee kulipa riba hata kama hizo biashara zimekufa,” anaeleza Kinshaga.

Pia, anasema mifuko mingi ya kusaidia biashara zinazohusiana na kulimo, zina lengo la kuweka mtegoni wajasiriamali wadogo wakati wakipatiwa mikopo na si kuwasaidia kwani vipaumbele vya mifuko huo ni usalama wa mifuko yenyewe.

“Wasimamizi wa mfuko wa dhamana wanahitaji kutafakari tena mifumo yao ili kuhakikisha kuwa wanatumikia kusudi la mifuko hiyo na kushughulikia shida halisi zinazounga mkono SMEs. Vinginevyo, fedha zitakuwa zinasaidia benki kuongeza faida wakati zinanufaisha kila mtu mwingine isipokuwa biashara zilizokusudiwa ambazo ni SMEs katika hatua za mwanzo na ukuaji," anasema.

Mjasiriamali mwingine katika mnyororo wa biashara ya kilimo ni Rachel Kingu ambaye pia ni mwanzishi wa Jore TZ ambayo inazalisha bidhaa za lishe zinazouzwa katika maduka makubwa katika mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, na Dodoma.

Uzoefu wa mjasiriamali huyo mwanamke katika kushughulika na mamlaka za serikali za mitaa kupata ufadhili uliotolewa kwa vikundi vya vijana na wanawake umemwacha na kumbukumbu mbaya.

Anaeleza kuwa alijihusisha na kikundi cha wanawake ambacho alikuwa ni Katibu wake katika kutafuta mkopo katika Mamlaka ya Serikali ya Mtaa ya Mvomero.

Anaelezwa kuwa alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wanakikundi wenzake kutokuona umuhimu wa kujitolea.

“Ukosefu wa kujitolea wa wanakikundi ulisababisha sehemu ndogo ya wanakikundi kupata wakati mgumu wa kurejesha makato ya mkopo huo kwa mamlaka hiyo. Kati ya wanawake 10 wa kikundi ni wawili tu ndio walishiriki kuendeleza mradi,” anaeleza.

Kingu anashauri serikali kuangalia upya utaratibu wa kutoa mikopo kwa vijana na wanawake huku kipaunbele kikiwa ni kusaidia mradi husika badala ya vikundi vinavyoomba mkopo.

Kampuni za Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) Tanzania na Sahara Ventures zimekuwa zikishirikiana kusaidia wajasiriamali wa lishe nchini kufikia utayari wa kiufundi na kuwekeza na hivyo kuchangia katika ajenda ya kitaifa ya maendeleo ya uchumi na lishe.

Wajasiriamali wanaojihisisha na biashara maalumu za lishe si tu wafanyabiashara wanaoongeza thamani katika kilimo bali pia wanasaidia Wananchi kuelewa umuhimu wa kula vyakula vya lishe na hivyo kukabiliana na utapiamlo.

Mwaka 2015, zaidi ya watoto milioni 2.7 nchini wenye umri chini ya miaka mitano walikadiriwa kuwa na udumavu na zaidi ya 600,000 walikuwa wanakabiliwa na utapiamlo mkali, ambapo 100,000 walikuwa katika hatua mbaya kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto na wanawake (UNICEF).

Kwa mujibu wa takwimu hizo asilimia 58 ya watoto waliodumaa inatoka katika mikoa 10 nchini na mikoa mitano inakabiliwa na tatizo la watoto wanaougua utapiamlo mkali nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz