Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhaba mafuta ya kupikia wawakutanisha Mkenda, Mtaka

1894ad02118b96ec9b4c98f0d12e5278.jpeg Uhaba mafuta ya kupikia wawakutanisha Mkenda, Mtaka

Sat, 5 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka ambapo wamejadili mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kupikia.

Katika mkutano wa viongozi hao ulioshirikisha pia wataalamu wa sekta ya kilimo wa mkoa huo, waziri Mkenda alisema Juni 13 mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kuhamasisha kilimo cha alizeti mkoani Singida.

Alisema hatua hiyo ni njia mojawapo ya kukabili changamoto ya upungufu wa mafuta inayosababisha nchi kulazimika kuagiza mafuta nje.

Alisema serikali itaanza safari yake kwa kuboresha huduma za ugani katika mikoa mitatu ya kielelezo ambayo ni Dodoma, Singida na Simiyu kwani ina fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususani alizeti na pamba.

Alisema hatua hiyo itaongeza chachu kubwa ya uzalishaji alizeti kama makakati muhimu wa kuelekea upatikanaji wa mafuta ya kutosha nchini.

"Tutaanzisha kampeni ya wakulima wakubwa, AMCOS na wakulima wote nchi nzima, tutawafungamanisha na wanaokamua mafuta ya alizeti ili wapate mikataba, tutahakikisha wanapata mbegu za kutosha kuhakikisha wanazalisha alizeti," alisema Mkenda.

Waziri Mkenda amempongeza Mtaka kwa usimamizi madhubuti katika sekta ya kilimo na kutoa kipaumbele kikubwa katika utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2021/2022.

Mtaka alisema kuwa timu hiyo ya mkoa aliyoingoza katika kikao hicho na Waziri wa Kilimo imekusudia kujibu utekelezaji wa hotuba ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2021/2922 kuhusu kukabiliana na changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kupikia nje ya nchi.

Alisema mkoa kupitia wilaya za Kongwa, Chemba na Kondoa zinazozunguka Jiji la Dodoma, ambazo ni wazalishaji wakubwa wa alizeti wanaingia katika jawabu la kukabiliana na changamoto ya tija ndogo katika uzalishaji wa alizeti.

Mtaka alisema lazima ifike mahala hata kama uagizaji wa mafuta nje ya nchi utaendelea, lakini nchi pia iwe na uhakika wa kuzalisha mafuta kwa wingi ikiwa ni pamoja na kuuza nje ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz