Kuadimika na kupanda kwa bei ya chakula cha kuku kumesababisha uhaba na kupanda kwa bei ya mayai katika majiji na miji mikubwa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Usomi Agriculture ambaye pia ni mtafiti mkuu katika sayansi ya wanyama, Dk Denis Mujibi, alisema kuna uhaba mkubwa wa mayai katika mji wa Kisumu na miji mingine mikubwa. “Kwa sasa mayai katika Jiji la Nairobi yanatoka Uganda na Tanzania.
Bei ya mayai imepanda kutokana na bei ya chakula cha kuku kupanda,” alisema Mujibi. Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ufugaji kuku ya Kenya, inayosambaza mayai kwa wauzaji wa rejareja katika eneo la Magharibi, Ronnie Hezron, alisema wafugaji wengi wadogo wameacha kazi hiyo kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.