Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugawaji pembejeo za pamba wapitiwa

7d27e39a462e759a6c11304a293869d3 Ugawaji pembejeo za pamba wapitiwa

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema wizara yake kwa sasa inafanya mapitio makubwa ya mifumo mizima ya kitaasisi, ambayo imekuwa ikitumika katika ugawaji wa pembejeo za kilimo hasa zao la pamba.

Profesa Mkenda alisema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa kikao cha ushauri cha mkoa wa Simiyu (RCC), kilichofanyika mjini Bariadi. Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wakulima kupata pembejeo kwa muda muafaka.

Kabla ya kuzungumza kwenye kikao hicho, alipokea malalamiko ya baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakiwemo wakuu wa wilaya, wabunge na wenyeviti wa halmashauri juu ya kutokuwepo kwa mbegu za kutosha kwa wakulima.

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi alisema kuwa kuna upungufu wa mbegu za kutosha kwa wananchi wao, na wananchi kulalamika mara kwa mara juu ya kukosa mbegu.

Kilangi alisema kuwa tatizo la mbegu na viuatilifu limekuwepo kila mwaka. Aliiomba serikali kuangalia upya mfumo ambao bodi ya pamba imekuwa ikitumia katika kugawa pembejeo hizo.

Profesa Mkenda aliwaagiza wizara hiyo kufanya uchambuzi wa mifumo hiyo ili iweze kupitiwa upya na kuboresha sekta ya kilimo.

"Nimekutana na malalamiko mengi sana juu ya usambazaji wa mbolea, mbegu na viuatilifu, kama wizara tunapitia upya mifumo hiyo, hasa kwenye zao la pamba ambalo wakulima wengi wamekuwa wakilalamika," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz