UZINDUZI wa usambazaji na ugawaji pembejeo za korosho kwa msimu wa 2023/24 umefanyika rasmi mkoani Mtwara kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima wa zao hilo kwenye maeneo mbalimbali yanayolima korosho nchini.
Akizungumza leo mkoani Mtwara, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema kwa msimu wa mwaka huu wamejiwekea lengo la kuagiza tani 49,000 salfa ya unga, viuatilifu vya maji lita milioni 3.130 na mabomba 52,000.
Hata hivyo amesema kuwa, viuatilifu hiyo ni vingi kuliko mahitaji ambapo kwa wastani wa mahitaji ya salfa kwa takwimu walizokuwa nazo ni kati ya tani 30,000 mpaka tani 35,000.
Aidha, mpaka sasa tayari tani elfu 8, 000 za salfa ya unga zimeshawasili nchini, viuatilifu vya maji lita milioni 1 pamoja na mabomba 5,000 kati ya hayo 5, 200 na katika suala la uhakiki ubora wa pembejeo hizo ni kwamba kila wakati wataendelea kuchukua sampuli kadri ambavyo pembejeo zinavyoendelea kuwasili.
‘’Lengo letu ni kwamba tunataka tujiridhishe katika suala hilo la ubora kabla ya pembejeo kusambazwa na kwenda kwa wakulima tunaanza kujiridhisha na ubora na ugwaji pembejeo utaanza kwenye meneo ambayo mikorosho inaanza kuchipua na zitagawiwa kwa wakulima waliyosajiliwa tu ndiyo watakaopewa pembejeo’’,
Amefafanua kuwa, katika tani elfu 8000 hizo za salfa ambazo tayari zimeshawasili nchini, zilizowasili katika ghala la kuhifazia pembejeo la Bodi ya Korosho mkoani humo ni tani 3,600 salfa ya unga, viuatilifu vya maji ni lita laki nane thelathini na sita mia tisa na tisini na mabomba 5,000.
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesisitiza suala la usimamizi wa zao hilo lifanyike kwa kila mdau ili wale ambao wana dhamira ya kuharibu utaratibu wa ugawaji wa pembejeo hizo kwa wakulimu waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amewataka wananchi mkoani humo kutambua kwamba, ruzuku hiyo inayototelewa na Serikali ni mchango wake katika kumpunguzia mkulima gharama ya uzalishaji wa zao hilo Nchini hivyo ni muhimu kwa kila mkulima kujiwekea akiba ya fedha kwa ajili ya kununua viuatilifu sokoni ili aweze kutosheleza mahitaji yake.