Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ufufuaji zao la mkonge kuinua kipato cha kaya

9b4f778a67c988d2e8a2749714f7c3b8 Ufufuaji zao la mkonge kuinua kipato cha kaya

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKONGE ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara nchini. Uzalishaji wa zao hilo duniani unakadiriwa kufikia tani 265,00 hadi 280,000 za nyuzi kwa mwaka na mahitaji ya dunia ni takribani tani 500,000 kwa mwaka kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2019 ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Tanzania ni mzalishaji wa pili duniani ambapo huzalisha wastani wa tani 36,000 hadi 38,000 za nyuzi kwa mwaka.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Kituo cha Mlingano, mkoani Tanga, Dk Catherine Senkoro anasema Tanzania ina eneo la hekta 44,123,561 sawa na asilimia 47 la eneo lote linalofaa kwa kilimo cha mkonge.

Lakini eneo linalolimwa ni hekta 64,029.73 sawa na asilimia 0.2 ya eneo linalofaa kwa kilimo cha mkonge. Anasema zao hilo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga, Mara na Pwani ambapo asilimia 60 ya mkonge wote hulimwa mkoani Tanga kulingana na taarifa ya Bodi ya Mkonge ya mwaka 2017.

“Uzalishaji wa mkonge hufanywa na wakulima wakubwa wapatao 22, wakulima wa kati na wadogo wapatao 7551 ambapo kiasi cha hekta 20,344 sawa na asilimia 31.8 zinalimwa na wakulima wa kati na wadogo,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Senkoro mwaka juzi, mkonge umeliingizia taifa fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani milioni 45.84 na Sh bilioni 11.74. Anaeleza kuwa pamoja na kwamba zao hilo ni la muhimu hapa nchini, takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji bado ni mdogo.

“Kwa mfano mwaka wa 2015, mkonge uliovunwa Tanzania ulikuwa takribani tani 40,000 za nyuzi. Hata hivyo katika miaka iliyofuata uzalishaji umepungua.

“Mfano katika mwaka wa 2018 uzalishaji wa mkonge ulikuwa tani 37,463.88 za nyuzi na tani 36,379.08 kwa mwaka 2019.

“Pia takwimu zinaonesha kuwa kwa wastani wakulima wadogo na wa kati huzalisha nyuzi za mkonge kiasi cha tani 0.8 mpaka 1.1 kwa hekta na wakulima wakubwa tani mbili mpaka 2.5,” anasema.

Anasema uzalishaji huo ni mdogo ukilinganisha na fursa ya uzalishaji wa hadi tani tano kwa hekta kwa mbegu chotara 11648 inayotumika sasa.

Kutokana na umuhimu wa mkonge katika uchumi wa taifa, zao hilo limetangazwa kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambapo mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza kituo cha utafiti Mlingano kuzalisha miche mingi ya kisasa ili kuwawezesha wakulima kunufaika.

Waziri Mkuu Majaliwa anasema serikali imeamua kuweka nguvu zote kwenye mkonge kwani zao hilo lilikuwepo na likafa.

Anasema uwepo wake katika kituo hicho cha Tari Mlingano na mkoani Tanga unaonesha dhahiri kuwa ni uamuzi wa serikali wa kulifufua zao hilo hivyo taifa litaokoa dola za Marekani zaidi ya milioni 245 mpaka milioni 250 zinazotumika kuagiza vifungashio vinavyotokana na zao hilo kutoka nje ya nchi.

Si hivyo tu baada ya kutoa agizo hilo, wiki iliopita Waziri Mkuu, Majaliwa aligawa miche iliyooteshwa na kituo cha Mlingano kwa wakulima wawili kituoni hapo kisha alieleza jinsi zao hilo linavyoweza kumtajirisha mkulima kwa kupata mavuno makubwa na fedha nyingi hata akilima kwenye eneo dogo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, ulimaji wa mkonge una faida kubwa kwa kuwa mkulima anaweza kuvuna tani moja kwenye hekta moja sawa na eka mbili na nusu hivyo kupata faida ya zaidi ya Sh milioni tatu baada ya kutoa gharama ya uzalishaji.

“Ili kuandaa eneo hilo mkulima anaweza kugharamia shilingi 50,000 za kukodi trekta la kusafisha eneo, atahitaji miche 1600 na kwamba kila mche atanunua kwa bei ya wastani ya shilingi 200.

“Hadi kipindi cha mavuno atakuwa ametoa takribani shilingi 560,000 zikiwemo gharama za vibarua wa kupanda, kupalilia na fedha za dharura zikiwemo za dawa.

“Kama makuzi yamekwenda vizuri kwenye hekta moja unaweza kuvuna tani moja, kiwango cha chini lakini unaweza kuvuna tani moja na nusu na kuendelea kwa kilimo hiki cha kawaida, hapo hujaweka utaalamu,” anasema.

Kwa maelezo ya Waziri Mkuu Majaliwa tani moja ya daraja la juu la mkonge inauzwa Sh milioni nne, daraja la chini Sh milioni 3.5, ikiondolewa na gharama za kuandaa shamba hadi kuvuna, kinachobaki ni faida.

Anasema lazima wakulima waambiwe kuwa kulima zao hilo linafaida kwani zao hilo likilimwa linavunwa kwa miaka 15.

Kutokana na umuhimu wa mkonge, Majaliwa anagiza halmashauri zote zinazolima zao hilo nchini zitenge eneo lisilopungua eka 10 kwa ajili ya kuandaa miche ili iwepo ya kutosha.

Pia agizo hilo limetolewa kwa wajasiriamali na taasisi zinazowekeza katika kilimo hicho ambazo zinamiliki mashamba makubwa ziwe na kitalu cha mbegu za mkonge kwa ajili ya wananchi ili kuonda upungufu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk Geofrey Mkamilo anasema mkonge ni miongoni mwa mazao saba ya kimkakati ambayo serikali imeweka nguvu ili kuchangia uchumi wa taifa.

Anasema ili kutatua changamoto za uzalishaji wa mkonge, Wizara ya Kilimo kupitia taasisi hiyo iliandaa mpango wa miaka mitano kuanzia 2019/20 mpaka 2023/24 wa uendelezaji wa zao la mkonge.

Lengo likiwa ni kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo ili kuchangia pato la mkulima na taifa. Malengo ya Tari ni kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mkonge, kubaini aina bora za mbegu za mkonge zinazoendana na mahitaji ya soko na mabadiliko ya tabianchi.

Pia kuhamasisha na kuelimisha maofisa ugani, wakulima na wadau wengine ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mkonge pamoja na kujenga miundombinu wezeshi na uwezo wa watafiti kwa ajili ya uendelezaji wa zao hilo.

Kuhusu uzalishaji wa miche bora ya mkonge anasema, Mlingano imeongeza uzalishaji wa miche bora ya mkonge aina ya chotara 11648 ambapo kufikia Oktoba mwaka jana eneo la ukubwa wa hekta 65 sawa na eka 162.5 limetolewa visiki na kusafishwa.

Aidha hekta 31.2 sawa na eka 78, ambazo ni sawa na asilimia 48 ya eneo lote lililosafishwa limepandwa miche ya mkonge 2,496,000.

“Mpaka kufikia Januari, 2021 jumla ya hekta 32.6 sawa na eka 81.5 zimepandwa miche ya mkonge katika maeneo ya Tari Mlingano hekta 31.2, halmashauri ya wilaya ya Muheza hekta moja sawa na eka 2.4 na Gaira hekta 0.4 sawa na eka moja.

“Pamoja na miche iliyokuwa shambani kabla ya Juni 2020, jumla kuu ni miche 2,672,000,” anasema. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tari, Dk Yohana Budeba anasema bodi ilitoa maagizo kituo cha Mlingano kizalishe mbegu bora na za kutosha ili wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa.

Lakini anasema kituo hicho mbali na kuzalisha mbegu bora kinatoa mafunzo kwa wananchi lakini pia ni shamba darasa la kusaidia kutoa elimu ya kilimo bora kwa wananchi.

Kwa upande mwingine Dk Senkoro anasema uzalishaji mdogo wa zao hilo kwa wakulima huchangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo upatikanaji mdogo wa mbegu bora, uelewa mdogo wa kanuni za kilimo bora cha mkonge, matumizi ya mbegu zenye uzalishaji mdogo, rutuba hafifu ya udongo na matumizi hafifu ya mbolea.

Anasema Tari Mlingano ina uwezo wa kuzalisha takribani miche bora ya mkonge 120,000 kwa njia ya maabara na imekuwa ikizalisha takribani miche 500,000 kwa njia ya kutumia vikonyo kwa mwaka.

Kiasi hicho cha mbegu ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya wakulima wadogo wanaohitaji miche 1,200,000 hadi 1,600,000 na wakulima wakubwa miche 10,000,000 hadi 12,000,000 kwa mwaka.

Mpaka sasa kituo hicho cha Mlingano kwa kushirikiana na Bodi ya Mkonge imetoa mafunzo kwa wakulima na maofisa ugani katika baadhi ya mikoa inayofaa kwa kilimo cha mkonge.

Mpaka Desemba mwaka jana wakulima 422 na maofisa ugani 840 katika mikoa hiyo walipatiwa mafunzo

Chanzo: habarileo.co.tz