Tanzania na ufaransa kupitia shirika lake la Maendeleeo AFD zimesaini mkopo wa masharti nafuu wa Shilingi bilioni 195 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa maji safi na usafi wa mazingira katika mkoa wa shinyanga.
Wakisaini makubaliano hayo jijini Dar es salaam katibu Mkuu wa Wizara ya fedha na mipango Emmanuel Tutuba amesema utekelezaji wa mradi huo wa maji unakwenda kuongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 katika manispaa ya shinyanga na watu zaidi ya laki tatu watanufaika na huduma ya maji safi na salama mkoani humo.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji mhandisi Anthony Sanga amesema , kukamilika kwa mradi huo pia kutasaidia kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 25,877 kwa siku hadi kufikia mita za ujazo 33,944 kwa siku.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajloui amesema kuwa lengo kuu la ufadhili huo ni kuboresha hali ya maisha ya wakazi pamoja na maendeleo ya kiuchumi kupitia upanuzi na ukarabati wa maji ya kunywa na huduma za usafi wa mazingira