Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Udom yabuni ufugaji nyuki kwa simu ya mkononi

Nyuki Wadogo.jpeg Udom yabuni ufugaji nyuki kwa simu ya mkononi

Fri, 27 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

. Ili kukabiliana na upotevu wa asali kwenye mizinga unaotokana na kuachwa kwa muda mrefu bila kuvunwa, Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) kimekuja na teknolojia mpya ya kumjulisha mfugaji wa nyuki kwa njia ya simu kuwa asali iko tayari kuvunwa.

Teknolojia hiyo iliyobuniwa na mwanafunzi wa Udom, Antoni Bairo inamwezesha mfugaji wa nyuki kupata taarifa zote zinazoendelea kwenye mzinga wake kwa njia ya simu.

Bairo amesema mizinga hiyo inafungwa kifaa maalum ambacho kinatumia umeme jua kinachounganishwa na simu ya mkononi ya mfugaji wa nyuki kitakachopeleka taarifa zote muhimu kuhusu kinachoendelea kwenye mzinga.

Amesema wafugaji nyuki ambao watafungiwa teknolojia hiyo wataingia makubaliano na Udom ambapo kama watashindwa kulipia gharama za awali watachukua robo ya mazao yatakayopatikana kwenye mzinga huo.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi, Bairo amesema teknolojia hiyo itamtaarifu mfugaji wa nyuki kuanzia siku ambayo nyuki wanaingia kwenye mzinga mpaka siku asali itakapokuwa tayari kuvunwa kwa njia ya simu yake ya mkononi.

Bairo amesema ni teknolojia rahisi na inatumika kwenye mizinga ya kawaida kwa ajili ya kumwezesha mfugaji wa nyuki kujua taarifa zote zinazoendelea kwenye mizinga yake aliyoiweka shambani au msituni.

“Wafuga nyuki wengi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kukuta asali yote imeshaliwa na nyuki kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu mzinga wake hivyo kukosa mazao ya asali ambayo anayategemea,” amesema Bairo na kuongeza kuwa;

“Lakini teknolojia hii itakuwa inampa taarifa kuanzia siku nyuki wanapoingia kwenye mzinga, watakapoanza uzalishaji wa asali na asali itakapokomaa mfugaji huyo wa nyuki atapata taarifa na kwenda kuvuna asali yake kabla haijaliwa na nyuki,” amesema.

Amesema teknolojia hiyo kwa sasa ipo kwenye majaribio na itakapokuwa tayari itapelekwa kwa wafugaji wa nyuki wa mikoa ya Dodoma, Katavi na Tabora kwa ajili ya kuona utendaji kazi wake na kama itakuwa na ufanisi mkubwa ndipo itakaposambazwa nchi nzima.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uzamili katika sayansi ya kemia amesema teknolojia hiyo itamwezesha mfugaji wa nyuki kupata mazao mengi ya asali kwa kuwa watakuwa wanavuna kwa wakati kabla asali hiyo haijaliwa na nyuki.

Amesema kwa kutumia mizinga ya kawaida ambayo siyo ya kisasa mfugaji wa nyuki ataweza kuvuna asali hadi lita 20 kwa mzinga mmoja tofauti na sasa ambapo huvuna kati ya lita mbili hadi tano kwa mzinga mmoja.

Ofisa Uhusiano wa Udom, Beatrice Baltazar amesema teknolojia hiyo imeshaanza kufanyiwa majaribio chuoni hapo ambapo kuna mizinga 20 ya nyuki inayotumia teknolojia hiyo na tayari wameshaanza kuvuna asali yake.

Amesema kwa sasa teknolojia hiyo ipo kwa ajili ya majaribio kwa kuangalia ufanisi wake na kama italeta mafanikio makubwa itapelekwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya kupata cheti na baada ya hapo itasambazwa kwa wafugaji wa nyuki na wakulima kwa ajili ya kutumika kibiashara zaidi.

Akizungumzia mnyororo wa thamani wa mazao ya asali, Mhadhiri wa Idara ya Baiolojia Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati, Dk Faith Mpondo amesema nta inayopatikana kwenye masega ya asali inaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo mishumaa na vifaa vya kutunzia urembo.

Amesema wakulima na wafugaji wengi wa nyuki wamekuwa wakitupa nta inayopatikana baada ya kurina asali bila kujua kuwa wanaweza kuitumia kutengenezea bidhaa zingine ambazo zitawaingizia pesa badala ya kuitupa.

“Sisi wafuga nyuki wa Udom huwa hatutupi nta inayopatikana baada ya kuvuna asali, tunatengenezea mishumaa, na kifaa vya kuhifadhia urembo, kuhifadhia miswaki na kuwekea maua ambayo baada ya kuiuza inatupa faida nyingine tofauti na ile ya kuuza asali,” amesema Dk Mpondo.

“Lakini pia tumefanya utafiti kwenye maabara zetu tumeona kuwa nta inaweza kukabiliana na vimelea vinavyoweza kushambulia ngozi hivyo ni nzuri pia kwa kutunza ngozi isishambuliwe na wadudu,” amesema.

Dk Mpondo amesema wanapovuna asali kwenye mizinga iliyopo chuoni hapo huwa hawatupi nta bali huwa wanaihifadhi kwa ajili ya matumizi mingine ambayo huwa yanawaingizia pesa.

Amesema vifaa na mishumaa inayotengenezwa na nta inadumu kwa muda mrefu na haiyeyuki kwenye joto la kawaida kwani huyeyuka kwenye nyuzi joto 62 hadi 64 ambalo halipatikani kwenye mazingira ya kawaida na hivyo kufanya bidhaa zinazotengenezwa kwa nta kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Amesema chuo hicho kipo tayari kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wafugaji wa nyuki ambao wanataka kuongeza thamani kwenye mazao ya nta ili waweze kujiongezea kipato kwenye shughuli zao za uchumi.

Mwenyekiti Taifa wa Jukwaa la Kuendeleza Ufugaji Nyuki Tanzania, Rudia Issa amesema teknolojia hiyo bado haijawafikia hivyo hawawezi kujua faida na changamoto zake ila watakapoijua ndipo wataisema kama inawafaa au haiwafai.

“Changamoto ya teknolojia huwa haipindi pindi huwa imenyooka, hivyo tutakapoifahamu vizuri mazuri na mabaya yake nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuisemea lakini kwa sasa sijui chochote kuhusu hiyo teknolojia,” amesema Rudia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live