Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Udhibiti wa mikopo chechefu waipaisha Benki ya DCB

Fri, 5 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Udhibiti wa mikopo chechefu mwaka wa fedha 2018 ni miongoni mwa sababu zilizoifanya benki ya biashara ya DCB kupata faida ghafi ya Sh1.6 bilioni ikilinganishwa na hasara ya Sh6.9 bilioni iliyopata mwaka 2017.

Akizungumza jijini Dodoma jana Alhamisi Aprili 4, 2019 katika hafla ya kutangaza matokeo ya uuzaji wa hisa, mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa amesema faida hiyo imeambatana na kukamilika kwa kazi ya uuzaji wa hisa.

Amesema manufaa hayo ni chachu ya ukuaji wa utendaji.

Ndalahwa amesema mafanikio mengine ni kupungua kwa gharama za uendeshaji na kuongezeka kwa ufanisi kupitia utoaji huduma kwa njia ya kidigitali, uboreshaji mtandao wa matawi na udhitibi mikopo chechefu.

“Ukiacha suala la kupata faida, mipango ya benki imekuwa ni kusimamia kikamilifu viashiria hatarishi na kuhakikisha benki inaendelea kuwa imara. Ikumbukwe kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwake ni kusaidia wajasiriamali wadogo kwa kutoa mikopo ya vikundi yenye masharti nafuu,” amesema Ndalahwa.

Hata hivyo, Ndahawa amezitaka halmashauri kuwekeza katika taasisi hiyo kwa sababu wote wana lengo la kuwainua wajasiriamali  ili kuweza kuanzisha biashara na kuondokana na umaskini.

Akifungua hafla hiyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha inafikisha elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya hisa ili kuwa na wateja wengi zaidi.

Dk Kijaji amesema wananchi wa kipato kidogo na cha kati wanatakiwa kufikiwa na huduma hiyo ili kuanzisha viwanda vigodo kwa lengo la kujikwamua na umaskini.

“Kwa sasa kuna changamoto ya umeme vijijini, lakini hadi mwaka 2020  huduma hiyo itakuwa imefika katika vijiji vyote, hivyo na nyie mnatakiwa kuwafikia wananchi ili ikifika mwaka huo waweze kuanzisha viwanda vidogo vdogo maeneo yao na kuwezesha kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025,” amesema Dk Kijaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz