Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Udart yaanika sababu za mabasi yake 70 kukwama

48468 Pic+udat

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya mabasi 70 ya Udart kufikisha mwaka tangu yashikiliwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), uongozi wa kampuni hiyo ya mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam, umeeleza mzizi mzima wa mgogoro huo.

Mabasi hayo yaliingizwa nchini Februari 16 mwaka jana kwa lengo la kupunguza msongamano wa abiria wanaotumia usafiri huo lakini yamekwama huku hali ya utoaji wa huduma hiyo ikizidi kuzorota siku hadi siku.

Wakati sababu kubwa ikidaiwa kuwa ni kodi ambayo Udart inadawa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), ikisema taratibu za uagizaji hazikufuatwa, wenye mabasi hayo wamefichua ukiukwaji huo.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, John Nguya, alieleza kuwa sababu kubwa ni kitendo cha iliyokuwa bodi ya kampuni hiyo kuamua kuyaagiza bila kikao cha kufikia uamuzi huo kuwa na wawakilishi kutoka serikalini wakiwamo Dart.

Nguya alisema kutokana na sababu hiyo, wameshindwa kuyakomboa kwa kuwa hawajapata kibali cha Dart ambacho kingewawezesha kulipa kodi na kisha kuyaingiza barabarani.

Mkurugenzi Mkuu wa Dart, Ronald Lwakatare alisisitiza kuwa Udart inapaswa kufuata utaratibu katika kuingiza mabasi.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuyataifisha ili kuyaingiza barabarani kwa lengo la kupunguza kero kwa abiria, Lwakatare alisema hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa itakuwa ni kuvunja sheria.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alipoulizwa kuhusu hatima ya mabasi hayo alisema bado wapo kwenye mazungumzo.

Yalivyoingizwa

Akielezea namna mabasi hayo yalivyoingizwa nchini, Nguya alisema bodi iliyokuwepo iliidhinisha kuyaleta baada ya kuona itafika wakati kutakuwa na uhitaji kutokana na wingi wa abiria.

“Kuna wakati ilikuwa ngumu hata kufuatilia ratiba ya mabasi kutokana na kujaa kupita kiasi. Kosa letu ni hilo tu tuliyaagiza bila kuushirikisha upande wa pili na hii ilitokana na wao kushindwa kuteua wawakilishi wao mapema kwenye bodi wakati kuna mambo mengine yalipaswa yaende katika biashara likiwamo hilo la kuongeza mabasi ili kutoa huduma iliyo bora,” alisema na kuongeza kwamba anaamini kuwa suala hilo litafikiwa muafaka.

Hata hivyo, alisema wakati ufumbuzi wa suala hilo ukitafutwa, kodi inaongezeka, abiria wanateseka na mabasi yanaharibika hivyo kuitaka Dart kuyaangalia kama yana viwango vinavyokubalika yaanze kazi ili kuyanusuru na kuwapunguzia wananchi adha ya usafiri.

Alisema uchache wa mabasi hayo unasababisha yaliyopo kutumika kuliko uwezo wake na hivyo kuharibika. Alisema mabasi makubwa yanatakiwa kubeba watu wasiozidi 155 lakini kwa hivi sasa yanabeba abiria 200 hadi 250. Mabasi madogo yanayotakiwa kubeba abiria 90, hubeba 100 hadi 150.

Ushindani wa kibiashara

Akizungumzia uwezekano wa kupatikana kwa mtoa huduma mwingine Nguya alisema hawapingi hilo kwa kuwa anaamini hatua hiyo itachangia kuleta ushindani katika biashara hiyo.

Hata hivyo, alisema jambo ambalo wamekuwa wakijiuliza ni jinsi Dart itakavyorudisha gharama za uwekezaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz