TAKWIMU mpya za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinaonesha kuwa Pato la Taifa la Tanzania (GDP) kwa bei ya sasa limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 85.42 (sawa na Sh trilioni 200) kwa mwaka 2023, ikiwa ni ishara kuwa sera za uchumi za Rais Samia Suluhu Hassan zinaleta mageuzi makubwa nchini.
Ongezeko hilo la pato la taifa ni kutoka Dola za Marekani bilioni 69.9 (sawa na Sh trilioni 163.5) kwa mwaka 2021 wakati Rais Samia alipoingia madarakani.
Takwimu hizo za IMF za Aprili, mwaka huu, zinaonesha kuwa pato la taifa la Tanzania huenda likaongezeka zaidi hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 136.09 (sawa na Sh trilioni 276) ifikapo mwaka 2028.
Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia ametekeleza sera rafiki kwa sekta binafsi, ambayo imeongeza kasi ya uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi nchini.
Kwa mujibu wa takwimu hizo mpya za IMF, Pato la Taifa la Tanzania mwaka huu ni kubwa kuliko nchi kadhaa ndogo za Ulaya, ikiwemo Croatia (Dola za Marekani bilioni 78.8), Lithuania (Dola za Marekani bilioni 78.3), Serbia (Dola za Marekani bilioni 73.9) na Slovenia (Dola za Marekani bilioni 68.1).
Kwa upande wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ni nchi ya sita kwa ukubwa wa pato la taifa.
Kwa mujibu wa takwimu za IMF, nchi 10 zinazoongoza kwa ukubwa wa Pato la Taifa Kusini mwa Jangwa la Sahara ni pamoja na Nigeria yenye Dola za Marekani bilioni 506.6, Afrika Kusini yenye Dola za Marekani bilioni 399.
Nyingine ni Ethiopia yenye Dola za Marekani bilioni 156, Kenya yenye Dola za Marekani bilioni 118.1, Angola yenye Dola za Marekani bilioni 117.8, Tanzania yenye Dola za Marekani bilioni 85.4 na Ivory Coast yenye Dola za Marekani bilioni 77.
Aidha, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yenye Dola za Marekani bilioni 69.4, Ghana yenye Dola za Marekani bilioni 66.6 na Uganda yenye Dola za Marekani bilioni 49.7.
Karika hatua nyingine, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa katika ujumbe wake kupitia akaunti ya Twitter alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa Tanzania kukua kiuchumi.
“Asante Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia uchumi wa Tanzania, unatuheshimisha,” alisema Msigwa katika ujumbe wake huo.