Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchumi wa Kidijitali: TCRA yawashika mkono wabunifu wa TEHAMA

Tehama Picggg TCRA yawashika mkono wabunifu wa TEHAMA

Mon, 4 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wabunifu katika tasnia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini Tanzania, sasa wataweza kutumia rasilimali adimu za Mawasiliano zikiwemo Namba fupi, masafa na kikoa cha.tz ili kukamilisha bunifu zao baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufunga makubaliano ya ushirikiano wa ubadilishanaji rasilimali hizo na Tume ya Sayansi na teknolojia (COSTECH) ambayo itapewa rasilimali hizo kwa niaba ya wabunifu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabiri Bakari alibainisha hayo kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere vya Maonesho ya viwanda na biashara ya SabaSaba alipofika kutembelea banda la TCRA.

“TCRA imejipanga vilivyo kuhakikisha kwamba wabunifu na wanafunzi ambao wana mawazo mazuri ya kuendeleza Uchumi wa Kidijitali,tunawawezesha”. alifafanua Jabiri na kuongeza kuwa, ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili unalenga kuwapatia wigo mpana zaidi wa ubunifu, vijana wanaoshiriki kuleta mawazo mapya katika TEHAMA na kwamba kupitia COSTECH, Mamlaka ya Mawasiliano itawapatia majukwaa na rasilimali adimu za majaribio.

“Tuna rasilimali namba, rasilimali masafa na dot tz; ambavyo kwa mujibu wa taratibu siku za nyuma ulikuwa unaweza kupata rasilimali hizi kwa kulipa leseni; kwa sasa kama wewe ni startup ‘mbunifu’ basi hizi rasilimali utapata bila gharama na hiyo ndiyo sababu tumetengeneza ushirikiano na wenzetu wa COSTECH” aliongeza.

Katika kuhakikisha mpango unafanikiwa TCRA pia imekubaliana na Tume ya TEHAMA kuwajengea uwezo wabunifu hasa vijana ili kuhakikisha wanatoa ushiriki wenye tija katika ukuzaji uchumi wa kidijitali. Katika kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa TCRA imeipatia jengo la ofisi Tume hiyo ili kuiwezesha kutekeleza malengo hayo ikiwemo kuimarisha mazingira na miundombinu itakayowasaidia wabunifu katika TEHAMA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dk Jabiri Bakari akikagua banda la Mamlaka kwenye viwanja vya maonesho ya biashara SabaSaba jijini Dar es salaam

Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kukuza ajira, kuwezesha upatikanaji wa bidhaa na huduma bila vikwazo vingi miongoni mwa faida za kuwajengea uwezo vijana wabunifu wa TEHAMA. Alibainisha kuwa mamlaka hiyo kwa sasa inajikita kuwajengea uwezo vijana kuanzia shule ya msingi ambako tayari Mamlaka inawezesha uanzishwaji wa klabu za kidijitali ili kukuza kizazi cha vijana wanaoiishi TEHAMA kwa vitendo.

Katika hatua nyingine Jabiri alisisitiza kuwa Mamlaka anayoisimamia itaendelea kusimamia ubora wa vifaa vya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano kutoka kwenye vifaa vyenye ubora.

“Sisi ni facilitators ‘wawezeshaji’ kwa hiyo unapokuja na uwekezaji mpya unaohusiana na mawasiliano au vifaa vitakavyowezesha muendelezo wa mnyororo wa mawasiliano tupo pale kufanya tathmini ya ubora wa kifaa hicho, kiwe kimetengenezwa nchini au nje” alibainisha Jabiri na kuongeza.

Alibainisha kuwa hadi sasa vifaa vya mawasiliano ya kiganjani vyenye uwezo wa kutumia intaneti katika teknolojia za 3G na 4G ni asilimia 28 pekee, akibainisha kuwa ikiwa uwekezaji wa utengenezaji vifaa vya mawasiliano hapa nchini utapatikana upo uwezekano mkubwa idadi ya watumiaji wa mtandao ikaongezeka kutoka asilimia 28 za sasa.

Awali mkuu wa Mkoa Amos Makalla akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegello walifika kwenye banda la Mamlaka hiyo na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na TCRA katika kusimamia huduma za mawasiliano nchini huku akiwatolea wito wananchi kuzingatia matumizi salama ya mitandao kwa ustawi na maendeleo.

“Nitoe rai tu kwamba watu tufanye kazi, mimi mwenyewe nimeshatumiwa tapeli akiigiza kuwa yeye ni mkuu wa mkoa, hivyo niwasihi wananchi wawe makini sana mara zote wanapopigiwa simu au kuona taarifa hasa za mikopo mtandaoni zinazowahusisha viongozi mbalimbali; tuwe makini”. alitahadharisha Makalla.

Katika aonyesho ya 46 ya biashara TCRA katika banda lake imeweka dawati linalowahudumia wananchi kwa kupokea na kuwapa taarifa mbalimbali juu ya matumizi ya huduma za mawasiliano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live