Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchumi, faida vyapunguza wafanyakazi 380 benki za biashara

9446 Pic+uchumi TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyakazi 381 wamepunguzwa na benki ili taasisi hizo kuendana na hali ya uchumi pamoja na kukabiliana na kupungua kwa faida.

Uchambuzi uliofanywa na Mwananchi kwa kupitia taarifa za fedha zilizotolewa na benki katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kati ya Juni 30, 2017 na Juni 30, 2018 zinaonyesha idadi ya wafanyakazi hao wamepunguzwa.

Baadhi ya benki zimejikita kupambana na tatizo la kupungua kwa faida kunakosababishwa na mikopo chechefu (isiyolipika).

Katika uchambuzi wa gazeti hili kwenye taarifa za benki 41 kati ya 58 zilizopo nchini zilizotoa taarifa za fedha za kipindi cha miezi sita iliyopita, umebaini benki hizo zimepunguza wafanyakazi 381.

Taarifa zinaonyesha kuna wafanyakazi 12,156 hadi Juni kulinganisha na wafanyakazi 12,537 katika kipindi kama hicho 2017.

Baadhi ya benki zilizopunguza wafanyakazi ni Access, Ecobank, Exim, ACB, CBA na CRDB.

Taarifa inaonyesha Benki ya Access iliongoza kwa kupunguza wafanyakazi 142 ikiwa na 634 hadi kufikia Juni 30, kulinganisha na 776 waliokuwapo Juni 2017.

Licha ya CRDB kuongeza matawi matano kati ya Juni 2017 na Juni mwaka huu, ilipunguza wafanyakazi 30. Hadi Juni mwaka huu ilikuwa na wafanyakazi 2,882 kulinganisha na 2,912 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Ecobank ambayo ilipunguza tawi moja na kubakiwa na saba katika kipindi hicho ilipunguza wafanyakazi 57. Benki hiyo ilikuwa na matawi manane. Licha ya wafanyakazi kupungua katika baadhi ya benki lakini NMB, Amana, UBA, Barclays na Azania ziliongeza watumishi.

Mkurugenzi mtendaji wa Ecobank, Mwanahiba Mzee alisema upungufu wa wafanyakazi ulitokana na kubadilisha mfumo wa uendeshaji. “Kampuni ilibadilisha mfumo wa ufanyaji kazi na kuweka mipya,” alisema.

Meneja masoko wa Access Bank, Sijaona Simon alisema wafanyakazi hao waliondoka baada ya kupata ajira sehemu nyingine.

“Tunafundisha wafanyakazi wengi na tunawaruhusu pale wanapokuwa wanapata kazi sehemu nyingine,” alisema.

Akizungumzia mwelekeo wa sekta ya benki, Mwanahiba alisema wanatarajia utakuwa mzuri.

“Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na hili linasababisha uboreshwaji wa miundombinu kama vile barabara ambayo inasaidia kukuza uchumi, viwanda, uzalishaji wa nishati endelevu na kuanzishwa miji mipya,” alisema Mwanahiba akitaja sababu zitakazosaidia kukua kwa sekta ya benki.

Chanzo: mwananchi.co.tz