Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchumi Zanzibar wakua, wafikia 6.5%

A762bd9f736b9ac0511f0b9cb849c277 Uchumi Zanzibar wakua, wafikia 6.5%

Wed, 15 Jun 2022 Chanzo: Habarileo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amewasilisha mpango wa maendeleo wa Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2022-2023 na kueleza kuwa uchumi wa Zanzibar umekua na kufikia asilimia 6.5 kutoka 5.2.

Dk Saada alisema hayo mbele ya Baraza la Wawakilishi na kutaja vipaumbele sita vinavyotarajiwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2020-2023 huku akitaja kuimarika kwa amani na utulivu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni sehemu ya maratajio makubwa ya mafanikio hayo ambayo yamefungua milango kwa wawekezaji kuwekeza.

Alivitaja vipaumbele hivyo ni kuwashajihisha na kuwavutia wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya bandari shirikishi huko Mangapwani.

Alisema ujenzi wa bandari hiyo utafanyika kwa njia ya kuwashirikisha wawekezaji katika sekta binafsi ikiwemo wa ndani na nje.

Alisema kuwa ujenzi wa bandari hiyo utahusisha miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa viwanda vya mazao ya baharini kama vile kusindika minofu ya samaki.

Aidha, serikali inaendelea na mikakati yake ya ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani na kusarifu mwani kilichoko Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba, hatua ambayo itasaidia kuimarisha kilimo cha mwani na kuwa mkombozi kwa wanawake.

Alisema uchumi wa buluu umepewa kipaumbele na kuwa miongoni mwa sekta itakayosaidia na kuongeza ajira kwa vijana na Sh bilioni 36 zimetengwa kwa kuwawezesha walengwa kufikia malengo hayo.

Alifahamisha kuwa ujenzi wa boti zitakazotumika katika uvuvi wa bahari kuu ni miongoni mwa vipaumbele vilivyowekwa katika uchumi wa buluu.

Dk Saada alitaja vipaumbele vinavyotarajiwa kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2022-2023 ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukifungua kisiwa hicho katika sekta ya uwekezaji na ukuaji wa utalii.

Chanzo: Habarileo