Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiweka mkakati wa kuongeza uuzaji wa nyama nje ya nchi, uchache wa machinjio za kisasa zenye ithibati ya kimataifa umetajwa kuwa changamoto inayorudisha nyuma jitihada hizo.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo kupeleka mifugo yao nchi jirani ili kufuata huduma za uchinjaji katika machinjio za kisasa zinazotoa vyeti hivyo ambavyo huruhusu uuzwaji wa nyama kwenye masoko ya kimataifa.
Hatua hiyo inachangia kupunguza mapato katika sekta hiyo kwa kuwa machinjio hizo za nje zinaingiza fedha zilizopaswa kuingia kwenye mzunguko wa fedha hapa nchini na hata nyama inayotokana na mifugo hiyo hutambulika kama imetoka katika nchi hizo zinakochinjwa.
Akizungumza na Mwananchi jana Desemba 7, 2023, Joseph Mwitatu ambaye ni mmoja wa wafugaji anayeuza nyama nje ya nchi amesema analazimika kutumia machinjio za Kenya kutokana na kukosekana kwa uhakika wa huduma hiyo hapa nchini.
“Nalazimika kupeleka mifugo yangu nje ya nchi kwa ajili ya kufuata machinjio yenye cheti, nimepata soko Dubai lakini ili niuze nyama kule ni lazima iwe imethibitishwa kuwa imechinjwa katika mazingira salama na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
“Huduma za machinjio na uchakataji wa nyama hazipo kwa wingi nchini, hali inayosababisha kuwa na gharama kubwa kwa sababu uhitaji nao umekuwa mkubwa baada ya masoko ya kimataifa ya nyama kufunguka,” amesema Mwitatu.
Changamoto ya gharama za uchakataji wa nyama inayouzwa nje ya nchi imeelezwa pia na mfanyabiashara Lameck Masanja, ambapo amesema kuwa wakati mwingine anaona ni heri auze mifugo hai kuliko kupambana na gharama hizo.
Akizungumzia hilo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Daniel Mushi amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kutoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ya sekta hiyo.
Amesema licha ya hatua ambazo Tanzania inapiga katika kufanya biashara ya nyama nje ya nchi huku kikuwa na ongezeko kubwa la kiwango cha nyama inayouzwa nje, bado uwekezaji unatakiwa kufanyika katika mnyororo wa thamani kwa kupanua wigo wa biashara.
Dk Mushi amefafanua kuwa endapo wafugaji wataendelea kufuata machinjio hizo nje ya nchi, Taifa litapoteza mapato ambayo yangezalishwa iwapo shughuli hizo za uchinjaji na uchakati zingefanywa ndani ya nchi na kutengeneza ajira.
“Serikali tunafanya mengi kuhakikisha mauzo ya bidhaa nje ya nchi yanaongezeka. Pamoja na jitihada hizo bado kuna changamoto ambazo tunahitaji kuzifanyika kazi ikiwemo hili la uchache wa machinjio zenye ithibati ya kuchinja nyama inayosafirishwa nje ya nchi.
“Ni jambo la kusikitisha wafugaji kwenda kuchinja mifugo yao nje ya nchi kwa kuwa wanafuata machinjio zenye vyeti au kuuza nje mifugo yao. Hili ni eneo ambalo linapaswa kufanyiwa uwekezaji mkubwa na tayari kuna kampuni zimeshaanza kuwekeza kwa kuanzisha machinjio hizi,” amesema Dk Mushi.
Mbali na hilo ameiomba sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya kuhifadhia nyama kwenye viwanja vya ndege vya Dar es Salaam na Kilimanjaro ili inayosafirishwa kwenda nje ya nchi iwe katika mazingira salama.
Dk Mushi pia ametumia fursa hiyo kuielekeza Bodi ya Nyama Tanzania kuhakikisha inaingia katikati ya wafugaji na wafanyabiashara wa nyama, kwa kuangalia suala la bei ili kupunguza biashara ya uuzaji wa mifugo nje ya nchi.
“Kuna mifugo mingi kutoka Tanzania inauzwa nchi jirani, huenda wafugaji wanavutiwa na bei lakini hii haina afya kwenye uchumi wetu hivyo ni muhimu tukaingia kati kuangalia nini kinaweza kufanyika mifugo hii iuzwe ndani.
“Haina maana Serikali tutazuia kwa sababu kama wamefuata taratibu zote hakuna kosa kuuza mifugo yao nje ila muhimu tuangalie nini kinawavutia huko kifanyike hapa ili biashara hiyo ifanyike nchini, sisi ndiyo tukauze nyama,” amesema Dk Mushi.
Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama, John Chassama amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha Tanzania inauza kiasi kikubwa cha nyama nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau katika sekta hiyo na kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo na utatuzi wake.
“Hili la machinjio nilimuunganisha huyo mfugaji na kampuni moja ambayo imeanza kutoa huduma hiyo hivi karibuni, tumekuwa tukikutana na wazalishaji wa bidhaa za nyama na wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa hizo nje ya nchi, lengo likiwa ni kuboresha biashara hii na kuondoa vikwazo vilivyopo,” amesema Chassama.
Hivi karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alieleza kuongezeka kwa soko la nyama nje ya nchi ambapo Saudi Arabia inahitaji tani 700,000 kwa mwaka na Tanzania imekaribishwa kwenye soko hilo.
Takwimu zinaonyesha mwaka 2021 nyama iliyouzwa nje ya nchi ilikuwa tani 1,774 lakini kutokana na jitihada zilizofanyika mwaka 2022 kiwango hicho kimepanda haki kufikia tani 14, 700 kilicholiingizia Taifa Sh147 bilioni.