Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuchochea uchumi

B54a75d17e5a5b42eef4db4ff95e9a23.png Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuchochea uchumi

Thu, 6 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Desemba 23, 2021 Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamis alisema wamepata baraka ya kupata mizigo mikubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, huku kwa tarehe hiyo akisema nje ya Bandari ya Dar es Salaam kulikuwa na meli 18 zinazosubiria kuingia, huku ndani ya bandari kukiwa na meli 13 zinazoendelea kushusha mzigo.

Kuwapo kwa meli hizo kunatokana kukamilika kwa awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam unaoendelea, mradi ambao umelenga kuboresha uwezo na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi kwa ajili ya manufaa ya wadau wote. Mradi huu utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 421.

Maboresho hayo ni pamoja na uimarishaji na uongezaji wa vina kwa Gati Namba 1 – 7 na ujenzi wa gati ya kuhudumia meli za magari katika Kijito cha Gerezani.

Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza uwezo wa uzalishaji wa mapato kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania pamoja na kutoa fursa za ajira kwa sekta binafsi na kusisimua maeneo mengine ya uchumi yanayozunguka eneo la Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bandari ya Dar es Salaam inaingiza zaidi ya Sh bilioni 70 kwa mwezi ikihudumia nchi za Malawi, Zimbabwe, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda na Uganda.

Dar es Salaam ni bandari kubwa yenye uwezo wa kuhudumia tani milioni 4.1 za bidhaa kavu kwa mwaka huku ikiwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni 6.0 ya vimiminika.

Ikiwa katika eneo bora zaidi za kuhudumia mizigo kwa nchi jirani ni kiungo na nchi nyingine za mbali za Mashariki ya Kati, Mashariki ya Mbali, Australia na Marekani.

Katika siku za karibuni kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika ikiwamo uchimbaji wake wa kina na ujenzi wa magati kumefanya Bandari ya Dar es Salaam kuvutia kampuni kubwa za usafirishaji duniani na kuleta meli kubwa zaidi za kisasa ikiwamo Tranquail Ace (IMO: 9561253) inayomilikiwa na Kampuni ya Mitsui. Meli hii ikiwa na magari 3,743 ambayo ni mengi zaidi kuwahi kusafirishwa kuja nchini, ilitoka Japan moja kwa moja.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi alisikika akisema kuwa meli hiyo imeandika historia mpya kutokana na kubeba shehena kubwa ya magari. Meli hiyo iliyotengenezwa mwaka 2009 na urefu wa mita 199.9 na upana mita 32.2 kwenda chini ilitia nanga Agosti 9, 2021 na kuanza shughuli ya ushushaji. Meli kubwa kuwahi kutia nanga nchini na iliyokuwa imebeba shehena kubwa ya magari ilitia nanga bandarini hapo mwaka 2018 ikiwa na magari 2,600.

“Leo ni siku nzuri sana katika historia ya TPA kwa kuweka rekodi mpya kwa kupokea meli kubwa na iliyobeba shehena kubwa zaidi kuja nchini. Hii haijawahi kutokea katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kubwa zaidi meli hii imetoka moja kwa moja Japan kuja nchini bila kupitia bandari nyingine.

“Kwa hiyo ni jambo jema dunia ikafahamu kwamba, Tanzania tuna bandari bora na ya kisasa yenye uwezo wa kupokea meli zote na ikazihudumia kwa wakati,” anasema Hamissi na kuongeza: “Katika inayoendelea kushushwa, magari yatasafirishwa kwa njia ya barabara kwenda nchi jirani na mengine 798 yanabaki hapa nchini.”

Ujio wa meli hiyo huku wastani wa asilimia 65 ya magari yake kwenda nchi jirani ni kuendelea kuaminika kwa bandari kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa. Wafanyabiashara wana uhakika wa mizigo yao kutolewa mapema na kusafirishwa kwa haraka zaidi kutokana na miundombinu ya usafirishaji barabara na reli kuwa bora.

“Mtaona ni jinsi gani sasa nchi zetu za jirani zinazotuzunguka zimeanza kutuamini, kati ya magari yaliyoingia asilimia 65 yanakwenda kwenye nchi hizo,” anasema.

Meneja Kampuni ya Inchcape Shipping Services, John Massawe anasema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba magari 5,200 ilitumia siku 20 na kwamba huo ni mwanzo wa kuleta meli nyingine kubwa zaidi.

Katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru, ilielezwa kuwa kumekuwa na ongezeko la shehena kupitia bandari zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kutoka tani 1,185,000 mwaka 1961 hadi kufikia tani 117,716,429 mwaka 2020/21.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema hatua hiyo imetokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyotekelezwa na serikali katika kuimarisha miundombinu ya bandari.

Profesa Mbarawa anasema TPA, inayosimamia jumla ya bandari rasmi 89 kati ya hizo bandari 12 ziko katika mwambao wa Bahari ya Hindi, 24 zipo katika Ziwa Victoria, bandari 19 katika Ziwa Tanganyika na bandari 11 katika Ziwa Nyasa wakati bandari nyingine 23 zinazohudumiwa na TPA lakini hazijaainishwa kwenye Sheria ya Bandari ya mwaka 2004. Bandari ya Dar es Salaam ndio lango kuu la uchumi nchini.

Anasema Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikifanyiwa maboresho mara kwa mara ili kufanya kazi kwa ufanisi tangu mwaka 1961 uliokuwa na uwezo wa kuingiza meli zenye urefu wa mita 145 – 175 na kina cha maji cha mita saba; baada ya maboresho makubwa sasa ina kina cha mita 14.5 na lango linaruhusu meli zenye ukubwa usiozidi mita 234.

Novemba 20 mwaka jana serikali ilisema imekwishaanza uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa awamu ya pili kwa ajili ya kuongeza kina cha maji kutoka mita 10 hadi kufikia mita 16 ili kuweza kuruhusu meli kubwa zenye urefu wa mita 305 na zenye uwezo wa kubeba kontena 8,000 kwa wakati mmoja kutia nanga bila kikwazo chochote.

Uboreshaji huo utakaogharimu kiasi cha Sh bilioni 219 mpaka kukamilika kwake utafungua bandari hiyo kwa kupokea mizigo mikubwa na kupunguza gharama za wasafirishaji.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mbarawa anasema kazi hiyo itakayochukua muda wa miezi 24 mpaka kukamilika kwake itawezesha bandari hiyo kuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia Watanzania pamoja na nchi zote za jirani za Rwanda, Burundi, Zambia na DRC .

Kuhusu uboreshaji wa bandari hiyo kwa awamu ya kwanza, Waziri Mbarawa anasema tayari serikali imekwisha kamilisha uboreshaji huo uliogharimu trilioni moja kutoka Gati 0 hadi kufikia 7.

Chanzo: www.habarileo.co.tz