Uboreshaji wa sera, sheria na mifumo ya uwekezaji nchini sasa unatoa fursa kwa watu wengi kuja kuwekeza nchini ikiwamo katika sekta ya bima.
Tanzania yenye idadi ya watu takribani milioni 60 hivi sasa, inafungua fursa kwa wawekezaji kuchangamkia fursa hizo katika nyanja tofauti.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya bima kwa Kampuni ya ICEA Lion General Insurance yaliyofanyika leo Machi 5 2024, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Tanzania ina mtaji wa kutosha wa watu licha ya kuzungukwa na mataifa mengine jirani, hivyo kuwa sehemu sahihi ya kufanya uwekezaji.
“Kuna mazingira mazuri na pia tunajivunia amani na utulivu unaohakikisha usalama kwa wawekezaji," amesema Profesa Mkumbo.
Amesema miongoni mwa sababu zilizoifanya ICEA Lion kumudu kufanya biashara nchini kwa miaka 25 ni ya mtaji wa watu na mazingira rafiki ya uwekezaji.
“Na sisi Serikali tunajivunia hili na kusimama nalo kuwa ni sehemu ya mafanikio kwa sababu na Watanzania wanapata ajira,” amesema Profesa Mkumbo.
Hata hivyo, amesema mazingira mazuri ya biashara ambayo Serikali inaweka katika sekta mbalimbali za uwekezaji ikiwamo ya bima kwa sasa, ndiyo inachangia sekta hiyo kufanya vizuri zaidi.
"Tunawahakikishia ushirikiano wa Serikali katika kuendelea kufanya biashara ili kutoa huduma bora za bima nchini."
Hata hivyo, Profesa Mkumbo ametoa wito kwa wadau zaidi, kampuni na taasisi mbalimbali za ndani naje ya nchi kuja kuwekeza nchini kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kufanya mageuzi bora ya kisera na kisheria kwa uendelevu wa biashara zao.
Amesema soko la Tanzania ni kubwa kwa sababu nchi inapakana na Jamhuri ya Demkrasia ya Congo (DRC), Burundi, Uganda, Kenya na Rwanda ambazo zina uhusiano mzuri kwa miaka mingi sasa.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Sagware amesema kuna maeneo mengi ya uwekezaji ambayo hayajaguswa vizuri.
"Kwa mfano, tuko katika mchakato wa kuanzisha mpango wa bima ya kilimo katika mazao ya kimkakati wa biashara, tunaelewa asilimia 70 ya watu wetu wanajishughulisha na mnyororo wa thamani wa kilimo, hivyo, katika mnyororo huo wa thamani kuna hitaji la ulinzi wa bima," amesema Dk Sagware.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema Serikali iko tayari kushirikiana na ICEA Lion na watoa huduma wengine wa bima ili kueneza elimu ya kuepuka hasara katika biashara zao.
"Hivi karibuni tumeshuhudia matukio kadhaa ya moto kwenye masoko yetu ya ndani na kusababisha hasara kubwa katika mitaji ya biashara.
“Kwa hivyo, Serikali iko tayari kushirikiana na wadau wengine kuelimisha watu juu ya bima kwa sababu watu wengi katika eneo hilo hawana bima," amesema Mpogolo.
Mkurugenzi wa ICEA Lion General Insurance, Jared Awando amesema watandelea kuwekeza nchini kwa lengo la kuwafikia mamilioni ya wateja walioko nchini.
“Ndiyo maana kampuni yetu imepanua ofisi zake katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma na kuingia Zanzibar hivi karibuni katika kuunga mkono uchumi wa buluu.
Katika sherehe hizo, kampuni hiyo ya bima pia imewazawadia wateja wake wa muda mrefu na wafanyakazi kwa ueledi wao.