Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ubora hafifu wa mazao watajwa kikwazo cha mikopo

Ccc4a916cd1d29be846b583608866cba Ubora hafifu wa mazao watajwa kikwazo cha mikopo

Mon, 29 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKWAMO wa baadhi ya wajasiriamali katika sekta ya kilimo kushindwa kupata mikopo ya kifedha katika benki umetajwa kuchangiwa na changamoto ya ubora wa mazao yanayozalishwa na kusababisha ukosefu wa masoko nchini.

Hayo yamesemwa mkoani hapa hivi karibuni na Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Benki ya NMB, Isaac Masusu,katika uzinduzi wa ‘Kizimba Business Model’ katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro .

Alisema mijadala ilikuwa mingi kuhusu njia bora kwa benki kuwezesha kutoa mikopo ya muda mrefu katika sekta ya kilimo na mfumo wa kilimo na kwamba, Kizimba Business Model imefungua njia ya kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Masusu alisema mfumo huo unawezesha vijana, akimama na wajasiriamali kuajiriwa katika sekta ya kilimo na mpango huo umejikita katika uwezeshaji upatikanaji wa ardhi ili kuitua kuzalisha mazao na kuongeza thamani.

“Kwa upande wa Benki ya NMB tumekuwa tukikwazwa na changamoto ya ubora wa mazao tunayozalisha na kiwango cha mazao yetu yanayozalishwa na wakati mwingine hata ukosefu wa masoko unatokana na mambo hayo yanayoweza kumvutia mnunuzi,” alisema Masusu.

Alisema moja ya kazi ya NMB ni kushirikiana na SUGECO kufungua njia kwa wakulima ili kuwawezesha kwa kushirikiana wadau wengine kubaini maeneo yanayosababisha benki kushindwa kutoa mikopo ya kilimo kwa makundi hayo.

“Benki ya NMB kwa sasa itaanza kutoa mikopo ya muda mrefu ambayo wakulima watanufaika nayo kutokana na aina ya uwekezaji katika sekta ya kilimo na fedha nyingi zinazohitaji katika kilimo zinahitaji muda mrefu na benki nyingi zenyewe zinahitaji kutoa fedha kwa muda mfupi na hiyo ndio mmoja ya sababu sekta ya kilimo kukwama katika kupata mikopo,” alisema Masusu.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema sekta ya kilimo imekuwa ikiajiri nguvu kazi nyingi nchini, lakini imekuwa haina tija.

Akitoa mfano, Profesha Mkenda alisema nchini Indonesia na nchi nyingine duniani, zao la mchikichi limekuwa na faida kubwa tofauti na Tanzania.

“Indonesia kwa hekta moja hupata tani 10 ya mafuta ya mawese wakati Tanzania hekta moja tumekuwa tukipata mafuta ya mawese tani 0.6 hiyo hivyo kuna kazi ya kuboresha kilimo chetu ili kuleta tija,” alisema Profesa Mkenda.

Chanzo: www.habarileo.co.tz