Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uandaaji viwango TBS unavyohimili kasi ujenzi wa viwanda

8cab7b78f98e9d90cb5becd8453ddf22 Uandaaji viwango TBS unavyohimili kasi ujenzi wa viwanda

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TANGU Serikali Awamu Tano iingie madarakani mwaka 2015, dhamira yake kubwa imekuwa ni ujenzi wa Tanzania inayotegemea uchumi wa viwanda.

Kwa kipindi chote tumeshuhudia jinsi, Rais John Magufuli anavyohimiza ujenzi wa viwanda, huku akitaka wizara na taasisi husika kuhakikisha zinaweka mazingira rafiki ya kuvutia uwekezaji.

Matokeo ya dhamira hiyo kila Mtanzania anaiona, kwani tunashuhudia viwanda vikijengwa kila kona nchini, huku Serikali ikionesha ukali wa watumishi au taasisi zinazokuwa kikwazo kwa wawekezaji.

Mtu asiyejua mabadiliko makubwa ya viwanda nchini, ni vyema leo atembelee mkoa wa Pwani wenye viwanda vingi nchini ataona namna Tanzania inavyoibuka katika sekta ya viwanda.

Lengo la hatua hiyo ya Serikali ni kuongeza ajira pamoja na pato la Taifa na kupunguza kuagiza vitu vingi nje, hali ambayo husababisha nchi kutumia pesa nyingi za kigeni.

Ili wawekezaji hao waweze kutimiza azma yao hiyo na nchi kufaidi matunda ya uwepo wao ni lazima bidhaa zinazozalishwa ziwe zinakidhi matakwa ya viwango.

Hiyo ni kwa sababu bidhaa nyingi huhitaji kufanyiwa vipimo na kutakiwa kukidhi matakwa ya viwango husika kabla ya kupelekwa sokoni.

Kwa msingi huo, katika biashara zinazohusisha nchi na nchi au mabara, kinahitajika chombo huru kisichoegemea upande wowote ili kukagua mtiririko wa uzalishaji, kufanya vipimo ili kuthibitisha ubora wa bidhaa au huduma husika.

Kwa hiyo uandaaji wa viwango ni moja ya maeneo muhimu katika safari ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda. Hapa nchini jukumu hilo lipo chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kupitia Kurugenzi ya Uandaaji wa Viwango.

Kiwango ni chapisho la kitalaamu linaloelezea matakwa ya msingi ya bidhaa na huduma au mifumo inayolenga kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi katika tasnia mbalimbali.

Kwa hiyo Kurugenzi ya Uandaaji Viwango jukumu lake kubwa ni kuhakikisha kuwa viwango vyote vinavyohitajika vinapatikana. Kwa mantiki hiyo uzingatiaji wa viwango na shughuli za udhibiti ubora ni mambo muhimu katika ukuaji wa viwanda, lakini pia ni sehemu ya biashara duniani, kwani huondoa vikwazo vya kibiashara na huleta ushindani wa kibiashara ulio sawa kwenye soko.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uandaaji wa Viwango wa TBS, David Ndibalema, anasema Kurugenzi ya Uandaaji wa Viwango ni moja kati ya kurugenzi nne za TBS, ambapo majukumu yake makubwa ni kuandaa na kutangaza viwango vya kitaifa katika nyanja zote za kiuchumi.

Pia, Ndibalema anasema Kurugenzi hiyo imekuwa na jukumu la kurekebisha viwango ambavyo tayari vimekwishaandaliwa kwa kuangalia kama bado vinafaa kwa matumizi.

Anataja jukumu lingine la kurugenzi hiyo kuwa ni kutoa mafunzo kwa wenye viwanda na wafanyabiashara kuhusu uzalishaji bora na utoaji huduma bora kwa kuzingatia viwango.

"Lakini pia kurugenzi hii inahusika na kukusanya na kutoa taarifa za viwango vya ndani na viwango vya nje, mfano kama kuna wafanyabiashara wanahitaji viwango vya kimataifa wanaweza kivipata hapa TBS kupitia kwenye maktaba yetu," anasema Ndimalema.

Anasema kwa kawaida kiwango huwa kinaandaliwa kwa kipitia kamati za kitaalamu (Technical committees) ambazo zinahusisisha wataalamu kutoka vyuo vikuu, taasisi mbalimbali zikiwemo za serikali na wizara, lakini pia kutoka kwa wazalishaji wenyewe kwa maana ya wenye viwanda na shirikisho la wafanyabiashara.

"Kutokana na uchumi wetu kuna maeneo yamepewa kipaumbele," anasema Ndibalema na kuongeza kuwa kuma Kamati za Kitaalamu takribani 109 ambazo zimegawanywa katika sekta tisa muhimu kiuchumi au za kipaumbele.

Anataja sekta hizo tisa kuwa ni Sekta ya Chakula na Kilimo, ambapo wataalamu wake wanaandaa viwango vya bidhaa za chakula na kilimo.

Sekta nyingine kwa mujibu wa Ndibalema ni sekta ya ngozi na nguo, sekta ya mazingira, sekta ya madini na teknolojia ya uchimbaji madini na sekta ya kemikali na bidhaa zake.

Maeneo mengine ni ya sekta ya kiufundi, ambapo kuna sekta ya ujenzi, sekta ya uhandisi umeme, sekta ya uhandisi mitambo na sekta ya jumla ya mambo ya kiufundi.

Anasema kila sekta inaandaa viwango kwenye hizo sekta zake. Kwa mujibu wa Ndibalema hadi mwishoni mwa mwaka wa fedha 2020 walikuwa wamefanikiwa kuandaa viwango 3,334.

Ndibalema anasema licha ya kuandaa viwango vya kitaifa, lakini pia wanashiriki katika uandaaji wa viwango vya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wa kikanda, anasema TBS ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini pia ni mwanachama wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO).

"Lakini pia tunashiriki SADC na huko kote lengo ni kuwianisha viwango. Tunapowianisha viwango tunatumia kiwango kile kile, kwa hiyo inakuwa rahisi kufanyabiashara kwenye maeneo hayo bila vikwazo.

Mfanao, bidhaa inayozalishwa hapa Tanzania inakuwa inakidhi kiwango ambacho kimewianishwa kikanda, hivyo inakuwa ni rahisi kufanyabiashara na kushindana kwenye soko la kikanda," anafafanua Ndibalema.

Aidha, anasema kupitia kurugenzi hiyo, TBS ni mwanachama wa Shirika la Viwango Duniani (ISO). Anasema ISO inashirikisha nchi wanachama kutoka duniani kote, hivyo na TBS inashiriki kwa karibu kwenye kamati za kitaalamu katika uandaaji viwango katika ngazi ya kimataifa.

"Na kutokana na uanachama wetu na ushiriki wetu tuna fursa ya kutumia hivyo viwango ambavyo vimeandaliwa kimataifa kwa sababu tunaviona vinafanana na mazingira yetu, hivyo tunavifanya kuwa vya kitaifa," anazidi kufafanua Ndibalema.

Kwa upande wa watumiaji viwango ambao wapo hapa nchini, anasema wanaweza kupata viwango hivyo kwa bei rahisi baada ya kurugenzi hiyo kuwa imevifanya vya kitaifa.

"Lakini kama wanataka kuvinunua kama vilivyo vya kimataifa, kupitia maktaba yetu wanaweza wakavipata na wakavinunua," anasema Ndimalema,"

Kuhusu utaratibu wa uandaaji viwango, Ndibalema anasema ni mfumo shirikishi, kwani kiwango kinaandaliwa kwa njia ya makubaliano baada ya kamati za kitaalamu kukaa na kujadili, kama kuna hitaji la kiwango fulani.

Anafafanua kwamba hayo mahitaji huwa wanayapata, aidha kwa kupata maombi kutoka viwandani, au kwa kuangalia mazingira ya soko na hata kuangalia sera za kitaifa, kwa kuangalia zimeweka mkazo eneo gani.

Anasema hitaji hilo linafanyiwa kazi ya awali na kikosi kazi na baada ya hapo inapatikana rasimu ya pendekezo la kiwango ambalo ni la kwanza na hujadiliwa na Kamati ya Kitaalamu.

"Ikishatoka kwenye Kamati ya Kitaalamu inapatikana rasimu namba mbili ambayo inajadiliwa katika Kamati ya Kisekta moja wapo kati ya sekta tisa nilizozianisha awali," anasema na kuongeza;

"Hiyo kamati ya kisekta ikishapitia rasimu hiyo ikaona inafaa inatoka na rasimu ya pendekezo ya kiwango namba tatu, ambapo pendekezo hilo sasa huwa linapelekwa kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni yao."

Anafafanua kwamba hiyo rasmu ya kiwango inawekwa kwenye tovuti ya shirika hilo, hapo wadau au mtu yeyote ambaye anaguswa na hilo eneo anaweza kupitia rasmu hiyo na kutoa maoni yake.

Rasimu ya kiwango hicho ikishapita kwenye hatua ya kupokea maoni ya wadau, kiwango hicho kinakamilishwa na kamati ya kitaalamu na baada ya hapo kiwango kinaidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi.

Baada ya hapo anasema inafuata michakato ya kukitangaza kwenye Gazeti la Serikali kama kiwango cha taifa baada ya kuidhinishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara na kuhakikiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Anasema kiwango kikishatoka inakuwa rahisi kutekelezeka. "Kiwango kikishakamilika huwa tunaendesha warsha au mafunzo ya kiwango hicho kama ni kipya kabisa ili kuwaelimisha wadau kuhusu kiwango hicho," anafafanua Ndibalema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz