Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tushike mkono tuwashinde Wachina kiuchumi

Samiaa Ikulu E Tushike mkono tuwashinde Wachina kiuchumi

Wed, 27 Dec 2023 Chanzo: mwanachidigital

Huku mtaani watu hawana elimu kubwa ya ufundi. Wengi wao hutumia akili ya kuzaliwa kujiendesha. Inawezekana meza ya mbogamboga au ya kuchonga vigoda ikawa ndio msingi wa maisha. Lakini Alihamdulilahi wengine wamejiongeza kwa semina au mafunzo ya ujasiriamali, hivyo wamepiga hatua ya kuvigeuza vipaji vyao kuwa kipato. Na kweli maisha yanabadilika; angalau fundi majiko na vinyozi wanaweza kuzalisha mali na kulipa kodi.

Biashara yoyote isiyo na ubunifu haiwezi kukua. Muuza mitumba anayefungua mzigo na kuutawanya mezani, anaweza kuuza kila shati kwa Sh2,000 na akapata faida ndogo.

Lakini namfahamu aliyejiongeza kwa kuyafua na kuyanyoosha mashati, akayafungasha kwenye vifungashio bora na kuyauza kwa bei mara tatu au tano na kupata faida kubwa katika mzigo mzima.

Hili ndilo ninalotaka kukwambia leo. Iwapo wajasiriamali wataongezewa uwezo na kuondolewa changamoto zilizo juu ya uwezo wao, bila shaka maisha ya uswahilini yangekuwa bora sana.

Wangeweza kuzalisha bidhaa bora na kutoa ajira kwa makundi mengine mtaani kama madobi, wafungasha bidhaa na wachuuzi. Kwa pamoja wangeweza kupandisha pato la Taifa na kuboresha hali ya uchumi kwa ujumla.

Kinachosikitisha ni kuona wabunifu wa Kitanzania hawatiliwi maanani kwa maana ya kuthaminiwa na kuongezewa uwezo. Bidhaa nyingi zinazotoka China na India zinaanza na wabunifu mmojammoja. Serikali zao zinawashika mikono katika sera ya viwanda vidogo hadi wakazalisha bidhaa za kuuzwa nje. Hapa nyumbani pamoja na kuwa tunalo Shirika la Viwanda Vidogo (Sido), bado hakuna mikakati ya kujenga uwezo wa wabunifu.

Ukubwa wa kampuni kubwa duniani ulianza na mtu mmoja au watu wachache. Historia inamtaja mzee Torakusu Yamaha kuwa mwanzilishi wa Yamaha Motors mnamo mwaka 1887.

Hakuna asiyejua umahiri wa Yamaha katika ulimwengu wa ushindani wa pikipiki duniani. Baada ya Yamaha ndipo utataja Honda, Suzuki, Kawasaki na wengineo. Kama mzee Torakusu angeachiwa peke yake tusingeyaona mazao ya ubunifu wake huku mtaani.

Bajaji tunazoziona leo kila kona ni mazao ya Mhindi mmoja aliyeitwa Jamnalal Bajaj. Alianza mchakato mwaka 1926 kwenye karakana yake ya nyumbani kule Mumbai. Alifanya kazi na ndugu zake, watoto wao pamoja na wajukuu, hadi wakawa na kundi la makampuni tofauti 40.

Ukiachilia mbali Bajaj tulizozizoea, pia wana kampuni za afya, ulinzi, nishati, bima na kadhalika.

Ni kawaida ya binadamu kupata maendeleo kutokana na changamoto zinazomzunguka. Katika nchi za Asia ni wazi akina Kawasaki na Bajaj kulikuwa na matatizo makubwa ya uchumi. Watu wa kawaida hawakuweza kumiliki vyombo vya usafiri vilivyotumia gharama kubwa. Na kwa sababu ya idadi kubwa ya watu, mabingwa wale wakaitumia shida hiyo kuwa fursa. Pia, kwa kuwa waliwezeshwa, wakashika masoko ya nchi zote duniani zenye changamoto kama zao.

Hapa kwetu tulizoea kuona wakati wa maonyesho ya Sabasaba, wabunifu wakija kuonyesha na kuuza majiko ya mkaa. Ilikuwa fursa kwa wakati ule, lakini kutokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya hali ya nchi tulitakiwa kubadilika.

Badala ya majiko ya mkaa, mafundi wetu wangeongezewa uwezo kitaalamu na kuhamia kwenye majiko ya umeme na gesi. Usishtuke, sikia mpaka mwisho uone kwamba umeme isingelikuwa changamoto hata kidogo.

Siku moja Mkurugenzi wa TBC, Dk Ayub Rioba akiendesha kipindi cha Adubini, aliwakaribisha wafua umeme wawili kutoka mkoani Njombe. Kila mmoja wao alianza kwa nguvu zake tangu miaka ya 80, lakini wakafanikiwa kuzalisha umeme wa njia za asili ulioweza kusaga na kukoboa nafaka.

Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli aliwaona na kuwaunganisha na Mamlaka ya Ugavi wa Umeme. Akatoa maagizo kwa mamlaka hiyo kuwashika mikono na kurudi na majibu ya kumalizwa kwa changamoto ya umeme. Kama mzee mmoja anafua kilowati 28 za umeme kienyeji, vijana mia moja wangefua ngapi kisasa?

Naamini iwapo mwendelezo wa mambo haya ungetiliwa mkazo, Watanzania wangeishika dunia.

Kwa nini nasema hivi? Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi zenye mahitaji makubwa ya bidhaa ndogondogo. Tunaona jinsi mzunguko wa bidhaa za nje unavyokuwa mkubwa siku hadi siku huku uswahilini.

Lakini pia kwa jinsi Watanzania wanavyotumia vipaji vyao kujipambanua, tuliona jinsi walivyokuwa wakiiga na kujifunza, hadi kufanikiwa kutengeneza bidhaa hizo kwa mikono yao.

Bongofleva ni mfano hai wa muziki unaopasua anga duniani kote. Muziki huu umesaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, umegeuza vipaji vyao kuwa fedha, na unaendelea kuongeza pato kwa Serikali. Wakati vijana walipokuwa wakijitafuta kufikia hapo, walianza kwa kuiga nyimbo za muziki wa disko kama ulivyo.

Mabadiliko yakawa yakija kwa awamu hadi kufikia utunzi na upigaji wa midundo. Kwa mtindo huohuo, wajasiriamali walianza kufungasha bidhaa za nje, lakini sasa wanatengeneza wenyewe tena kwa kutumia rasilimali zetu.

Bidhaa wanazotengeneza kama sabuni ya vipande na ya maji, dawa ya kusugulia masinki, mafuta ya karanga, alizeti na nazi ni za Kitanzania. Bila shaka hawa wangeongezewa uwezo wangekuwa kwenye ushindani na bidhaa za nje.

Chanzo: mwanachidigital