Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunahitaji mkakati wa muda mrefu wa umeme

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mradi wa umeme unaoendelea kwenye Bonde la Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2021 au 2022 utaliletea taifa umeme wa megawati 2100. Tuzungumzavyo, tunao umeme wa kipindi cha mpito wa megawati 1,602.

Megawati 1,602 zilizopo tukijumlisha na 2,100 za Stiegler’s Gorge tunakuwa na umeme wa megawati takribani 3,700.

Umeme huu ni mwingi sana? Jibu la swali hilo kwa sasa linaweza kuwa ndiyo lakini baadaye, labda baada ya miaka mitano linaweza kuwa hapana.

Muda huu ambapo tunazo megawati 1,600, matumizi yetu katika nchi ni megawati 1,400 hivi, kwa hiyo tunakuwa na bakaa ya megawati 200 hivi, lakini hali hii haitakuwa ya kudumu kama hakuna juhudi za kuleta umeme mwingine. Juhudi za serikali katika mradi wa Stiegler’s Gorge ambazo mimi naweza kuziita mpango wa muda wa kati, siyo za kubeza hata kidogo.

Mpango wa muda mrefu wa uzalishaji

Kama tunataka kuzungumzia uzalishaji wa umeme kupitia mpango wa muda mrefu lazima tuiangalie Tanzania ijayo kwa miaka 50 – 500 hivi. Sisi tunaoishi leo hatuishi kwa ajili yetu, tunaishi kwa ajili ya vizazi vya wajukuu wetu na mipango yetu inapaswa kuzingatia hali zetu za uchumi na vipaumbele muhimu vya sasa, lakini kila mara miradi mikubwa izingatie taifa la miaka ijayo.

Mradi wa Stigler pamoja na kupondwa na baadhi ya mashirika ya kimataifa na nchi kadhaa wahisani, bado ni wa lazima kwa kipindi cha kati. Sababu za kimazingira zinazotolewa na watu wasiotaka mradi huo zina ukweli kiasi fulani, lakini kiuhalisia nchi yetu inahitaji kupiga hatua mbele. Inahitaji kujenga viwanda, miundombinu inayotumia umeme na mambo kama hayo, bila umeme wa uhakika na wa kutosha, miradi hiyo haitawezekana.

Nchi yenye umeme wa ziada wa megawati 200, ambayo miaka kadhaa iliyopita iliishi kwenye nakisi kubwa ya umeme na kupoteza fursa nyingi za uwekezaji na upotezaji wa fedha nyingi kutokana na gharama kubwa za kuzalisha umeme wa mafuta – ni nchi inayopaswa kufanya haraka kukamilisha miradi mingine ya umeme ukiwamo huu wa Stieglers.

Miradi ya kupiganiwa itakuwa kwenye mfumo wa muda mfupi, muda wa kati na mpango wa muda mrefu. Mipango hii inapaswa kuangalia hali halisi ya nchi kuliko maoni ya wahisani, maana hata huko Ulaya na Magharibi, walijenga miundombinu ya umeme wa uhakika kwanza ndipo wakaendelea kufanya uwekezaji wa uhakika kwenye sekta zingine.

Baada ya Stieglers Gorge

Tukipata umeme wa Stieglers tutakuwa na ahueni kubwa ya umeme. Je, jambo hilo ni la kudumu? Hapana! Kunahitajika mikakati ya muda mrefu inayopaswa kupangwa sasa na kuanza kutekelezwa mara moja kwa kutengewa fedha polepole.

Kwa sasa taifa letu linategemea umeme wa maji kwa kiasi kikubwa, takribani asilimia 70 ya umeme unaozalishwa hapa kwetu unatokana na maji. Tumesahau kuwa maji huisha? Ndiyo maji huisha. Maji siyo kitu cha kudumu, ni rasilimali ambayo hutoweka pia, yaani, mabwawa yetu kama Mtera na mengineyo, ipo siku yanaweza kutoweka.

Mito muhimu kama Ruvu, iko siku haitakuwepo tena. Kihistoria, yako maziwa na mito mingi ambayo leo hii siyo mito wala maziwa, ni majangwa.

Ni muhimu basi, kama huo ndio ukweli, tukalielekeza taifa katika kuanza uwekezaji wa umeme wa upepo na jua. Walau upepo ni kitu cha uhakika, jua ni kitu cha uhakika pia.

Na kadri miaka iendavyo, hali ya uoto wa asili inatoweka na jua linazidi kutuchoma na kutumulika kwa ukali zaidi. Wakati tunalia jua ni kali tulitumie kama fursa, tujijengee mitambo mikubwa kila kanda kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kutosha siku zijazo.

Umeme wa jua unahitaji kuwa na vifaa vya kutosha kwenye maeneo mapana ili kuupata kwa wingi unaohitajika. Umeme huu ni rahisi kuuvuna hata nyakati ambazo mvua inanyesha kwa sababu paneli zinazopokea nishati hiyo kutoka kwenye jua zinahitaji mwanga peke yake kutengeneza umeme.

Tulilinde taifa lijalo

Mambo haya yanawezekana, yanawezekana tukiendeleza nia yetu ya kuondoa giza kwa kizazi kijacho mara baada ya kuwa tumetatua matatizo yetu ya umeme kwa wakati wa sasa.

Ndiyo maana tunalo jukumu la kuangalia mbele zaidi, maana umeme ni maisha na maisha ni umeme. Serikali yetu inaweza kuanza kutenga wastani wa Sh200 bilioni kila mwaka wa fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye utafiti na ununuzi wa vifaa na mitambo mikubwa ya umeme wa jua na upepo.

Ndani ya miaka 20 ijayo tunaweza kuwa tumewekeza Sh4 trilioni ambazo zitaanza kutupatia umeme wa uhakika unaotokana na upepo na jua katika mikoa mingi ya Tanzania. Umeme huu ukiongezwa na ule wa maji na gesi, nchi yetu itakuwa na uhakika wa kukaribisha kila aina ya uwekezaji na wananchi wetu itafikia wakati watafanya kazi saa 24 kwa sababu umeme utawaka kila mahali na ukuaji wa teknolojia utakuwa wa juu sana.

Julius Mtatiro ni mchambuzi na mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera; pia ni mtafiti, mfasiri na mwanasheria. Simu; +255787536759 Baruapepe: ([email protected])



Chanzo: mwananchi.co.tz