Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunaenda vyema kwenye madini, bado misitu

5d281b384537e6ef1dcee2d016c7a5c2 Tunaenda vyema kwenye madini, bado misitu

Tue, 8 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TANGU Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha nchi inanufaika na madini yake zinatia matumaini sana. Kumekuwa na habari njema kila kukicha namna mapato yanavyoongezeka katika eneo hilo.

Hata kwenye rasilimali za majini, tumekuwa tukifanya vyema pia. Kwa sisi wakazi wa Dar es Salaam, tumekuwa tukishuhudia ongezeko la upatikanaji wa samaki kutoka maji baridi, hususani sangara huku bei yake ikiwa rafiki kwa muda mrefu, kilo ikiuzwa kati ya Sh 6,000 na 7,000 kwa rejareja. Bei hii kwa maeneo mengi ya Dar es Salaam, ni sawa au pungufu ya bei ya kilo ya nyama.

Hatua zilizochukuliwa zinaonesha pia kwamba tumekuwa tukifanya vyema kwenye vivutio vyetu kama hifadhi zetu za taifa, tukielezwa kuhusu ongezeko la watalii na matumaini ni kwamba janga la corona litakapoisha kabisa duniani, idadi ya watalii itaongezeka maradufu.

Tatizo, kwa mtazamo wangu limebaki kwenye rasilimali misitu ambako katika maeneo mengi ya nchi yetu kumekuwa na uvunaji holela kiasi cha wajanja wachache kunufaika na rasilimali hizo na kusababisha uharibifu.

Mbali na uvunaji holela, hususani katika misitu ya vijiji inayofanya asilimia karibu 45 ya misitu yote nchini (zaidi ya hekta milioni 20), kikubwa ambacho kimekuwa kikimaliza misitu ni kuigeuza kuwa mashamba.

Ni kweli, tunahitaji maeneo ya kulima lakini tunapaswa kutumia teknolojia zaidi kwenye kilimo ili tuwe tunalima eneo dogo na kupata mavuni makubwa kuliko kumaliza misitu kwa kugeuza mashamba kwani misitu pia ina faida kubwa kwa mwanadamu.

Mbali na kutoa mazao ya misitu kama mbao, magogo, fito, kuni, mkaa na dawa, misitu hutunza vyanzo vya maji, huvuta mvua, hunyonya hewa ukaa na kusaidia kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuwa makazi ya viumbehai wa aina mbalimbali wakiwemo nyuki na kadhalika.

Hivi karibuni, nilikuwa miongoni mwa waandishi tuliotembelea baadhi ya vijiji ambavyo vimekuwa vikiendesha Usimamizi Shirikishi wa Misitu (Community Based Forest Management-CBFM) kwa maana ya kufanya uvunaji endelevu na kutumia mapato katika ulinzi shirikishi wa misitu inayozunguka vijiji vyao.

Vijiji hivi, kama vile Nanjirinji (Kilwa), Mlilingwa (Morogoro), Ulaya Mbuyuni (Kilosa) na vingine kadhaa vimekuwa vikiingiza mamilioni ya pesa kupitia rasilimali misitu kwa njia ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM)

Tafiti zilizoendeshwa kitaalamu na wasomi wa vyuo vikuu katika vijiji hivyo, zimeonesha pia kwamba uharibifu wa misitu umepungua sana kulinganisha na vijiji ambavyo havifanyi USM.

Kinachofanyika katika vijiji hivyo kwanza ni kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji kama vile kutenga eneo la makazi na huduma za kijamii, eneo la mashamba, eneo la mifugo, eneo la msitu kisha ndani ya eneo la misitu kunatengwa eneo dogo la takribani asilimia 10 hadi 15 la msitu wote kwa ajili ya uvunaji wa rasilimali misitu kwa miaka yote huku asilimia 85 au zaidi ya msitu unaozunguka kijiji ulikuwa haliguswi daima.

Waandishi tulielezwa kwamba vijiji hivyo vimekuwa vikiingiza mamilioni ya pesa kama ushuru kutokana na uvunaji wa misitu huku vikichangia pia asilimia 10 ya mapato yao kwa halmashauri husika. Kijiji kama Nanjirinji, kwa mfano, ambacho kilikuwa na mapato ya wastani wa shilingi milioni 10 kwa mwaka miaka ya nyuma, baada ya kuanzisha USM mapato yalipanda hadi zaidi ya shilingi milioni 100 kwa mwaka. Wananchi baada ya kuona manufaa ya msitu wao wakawa ndio walinzi namba moja kuhakikisha hakuna mtu anachezea msitu.

Waandishi pia walijionea miradi mbalimbali ambayo imefanywa na wanavijiji katika maeneo yote yanayoendesha USM kama vile ujenzi wa madarasa, uchimbaji wa visima, vyoo vya shule, ofisi za kisasa za vijiji, kulipia wanakijiji bima za afya, kusaidia gharama za matinbabu na uzazi kwa wajawazito, kusaidia wanafunzi wanaofaulu na kadhalika na kadhalika.

Kwamba, kukiwa na usimamizi shirikishi wa misitu na elimu ya kutosha ikatolewa kuhusu namna ya kuvuna raslimali hizi kwa njia endelevu kama ambayo imetolewa katika vijiji nilivyovitaja na vinginevyo, hakuna sababu ya kufikiria kupeleka milioni 50 kwa kila kijiji kama alivyowahi kuahidi Rais John Magufuli wakati anagombea urais na kisha kubadilisha nia hiyo. Vijiji vyenye misitu

Watu wengi hawajui kwamba mkaa unaweza kuvunwa kwa njia endelevu, faida kubwa ikapatikana bila kuathiri misitu. Kwanza ieleweke kwamba kwa mujibu tafiti zilizopo, wakazi wengi wa mijini, wataendelea kutumia mkaa kwa ajili ya kupikia kwa miongo kadhaa kabla ya kuanza kutumia nishati mbadala.

Takwimu za Msingi za Hewa Ukaa (Forest Reference Emission Level-FREL) za mwaka 2016 zinaonesha kwamba asilimia 96 ya kaya hapa nchini zinatumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.

Bila shaka jiji la biashara la Dar es Salaam tunaweza kusema lina wakazi wengi wenye kipato cha kati lakini bado takwimu zilizopo zinaonesha kwamba asilimia 91 ya kaya katika jiji hilo bado zinatumia mkaa kwa kupikia na kwamba takribani asilimia 50 ya mkaa wote unaozalishwa nchini unatumika Dar es Salaam!

Kwa mujibu wa takwimu hizo, zaidi ya tani milioni 2.3 za mkaa zinatumika kwa mwaka hapa nchini na mchango wa sekta ya mkaa kwenye uchumi wa nchi ni takribani Sh trilioni 2.2 kwa mwaka kiasi ambacho hakuna zao la biashara linalofikia kiwango hicho.

Kutokana na kutokuwa na uzalishaji wa mkaa usio endelevu, mapato yanayopotea kwa mwaka ambayo yangeliingia kwenye serikali za vijiji, halmashauri hadi serikali kuu yanatajwa kuwa Sh bilioni 220 kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu zilizopo. Kwa nini nchi nzima isijikite kwenye USM ili pesa hizi ziingie kwenye kibindo cha serikali?

Je, nini kinafanyika katika uzalishaji mkaa endelevu kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzaia (TTCS)? Kinachofanyika kama ilivyodokezwa hapo juu kijiji kinatenga eneo la mistu la lisilozidi asilimia 15 kwa ajili ya mkaa. Katika eneo hilo, kunatengwa vitalu vya mita 50 kwa 50 kwa kutumia vipimo vya GPS.

Vitalu hivi huvunwa kwa kuruka kwamba kama kitalu A kinavunwa leo, B kinarukwa hadi C na B kitarejewa baada ya miaka 12 katika mzunguko wa miaka 24 ambapo kitalu kilichokatwa leo miti huwa kimerejea kuwa msitu mkubwa tena.

Miti yenye sifa tu ndio inayovunwa kwa ajili ya mkaa na pia katika kitalu kinachovunwa, miti inayofaa kwa mbao inaachwa au iliyo katika vyanzo vya maji au makazi ya viumbe hai pia haiguswi.

Uzalishaji wa mkaa pia hufanyika kwa kutumia matanuri yaliboreshwa ambayo hutoa mkaa mwingi na mzuri.

Kutokana na manufaa ambayo wavijiji wamekuwa wakipata huku wakivuna mkaa bila woga kwa mujibu wa taratibu, wamekuwa ndio walinzi wakubwa wa misitu yao.

Vijiji 30 katika mkoa wa Morogoro na vingine kadhaa katika wilaya ya Kilwa vinavyotekeleza USM ni mfano mzuri wa kuigwa. Mimi hutamani Rais Magufuli avitembelee ili kuona manufaa ya misitu kwa vijiji hivyo na taifa kwa ujumla.

Baada ya mradi huo wa TTCS kumalizika na kuonesha mafanikio makubwa kwa vijiji vinavyouendeleza, kumeanzishwa mradi mwingine wa Kuhifadhi Misitu na Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu nchini (Conserving Forests through sustainable Forest- based Enterprise Support in Tanzania - CoForEST).

Malengo ya mradi huo ulioanza Desemba mosi mwaka jana na kutarajiwa kumalizika Novemba 30 mwaka 2022, ni kuimarisha usimamizi shirikishi na endelevu wa msitu ya asili katika kufanya mazao ya misitu yachangie mnyororo wa uchumi na wakati huo huo kusaidia kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Wakati habari hizi njema tumekuwa tukiziandika sana na kudhani wasaidizi wa Rais watavitembelea vijiji hivyo na kisha kueneza elimu ya uvunaji endelevu wa rasilimali misitu katika vijiji vingine nchi nzima kama ilivyofanyika kwenye masoko ya madini, wao wamekuja na mpango unaonekana kuvikwaza hata vijiji vilivyokuwa ‘vikichanua’kutokana na mtumizi endelevu ya -raslimali misitu.

Serikali imekuja na kanuni mpya za misitu kupitia tangazo namba 417 (GN 417) ambalo ni kama limeondoa madaraka ya vijiji kujipangia namna ya kuvuna na kusimamia misitu iliyo katika maeneo yao.

Sasa kumewekwa hata bei elekezi ambayo pia imekuwa kikwazo kwa baadhi ya vijiji. Bei hiyo husababisha wafanyabiashara kusita kwenda kwenye vijiji vilivyo mbali na soko na kwenda vilivyo karibu au kwenye maeneo wanayovuna mkaa kwa njia holela.

Inawezekana hatua hiyo ililega vijiji ambavyo haviendeshi USM ambavyo ndivyo vingi, lakini kwa mtazamo wangu kilichotakiwa ni wahusika kwenda katika vijiji vinavyoendesha USM na kusikia manufaa makubwa na kisha kuanzisha utaratibu huo Tanzania nzima kwenye vijiji vyenye misitu inayofaa kuendesha utaratibu huo.

Serikali inapaswa pia kuvuna ujuzi au kushirikiana na asasi za kulinda misitu ya asili zisizo za kiserikali ambazo zimekuwa zikiendesha miradi hiyo ya uvunaji endelevu katika vijiji mbalimbali TTCS na sasa CoFoeEST). Asasi hizo ni pamoja na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo (MCDI) na mengineyo.

Gharama za kuanzisha miradi kama inayoendeshwa katika vijiji mkoani Morogoro ni Sh milioni 12 tu ambazo zinarudi muda mfupi baada ya uzalishaji kuanza.

Chanzo: habarileo.co.tz