Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume yasema sabuni ya Mo Cleansoft imeiga jina

90085 Sabuni+pic Tume yasema sabuni ya Mo Cleansoft imeiga jina

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni ya Keds Tanzania Co. Ltd imeshinda shauri lake dhidi ya kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL) ambayo inadaiwa kuiga nembo ya bidhaa ya sabuni ya unga ya Kleesoft.

MeTL inadaiwa kuipa sabuni yake jina la Mo Cleansoft ili kuwepo mfanano na jina la Kleesoft.

Kutokana na ushindi huo, bidhaa za sabuni ya Mo Cleansoft ambazo zilizuiwa ghalani wakati shauri hilo likisikilizwa, sasa zinachukuliwa kama bidhaa `bandia’.

Alipotafutwa kuhusu uamuzi huo, mwanasheria wa MeTL, Catherine Kisasa hakutaka kuzungumza lolote.

Shauri hilo lilifunguliwa Tume ya Ushindani (FCC) na kampuni ya Keds Tanzania na kusikilizwa na kamati ya usikilizaji wa shauri hilo. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe watatu ambao ni Joseph Mkizungo (mwenyekiti), Roselyn Nyanda na Josephat Kilato.

Madai ya msingi ya Keds Tanzania yalikuwa ni kuwa kampuni ya MeTL iliiga vitu mbalimbali vilivyomo kwenye bidhaa yao, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Bidhaa (Merchandise Act).

Mambo mengine yaliyolalamikiwa ni kufanana kwa rangi na mwonekano wa vifungashio vya sabuni hizo mbili-- Kleesoft na Cleansoft-- huku Keds Tanzania wakiwatuhumu washindani wao kuwa wameiga rangi na muundo wa vifungashio vyao pamoja na kaulimbiu yao ya “Sabuni Kidogo, Nguvu Zaidi.”

Jambo jingine walilolalamikia ni mfanano wa matamshi ya majina ambao wanadai umekuwa ukiwachanganya walaji.

Matamshi ya majina ya Kleesoft na Cleansoft yanafanana, jambo ambalo wanadai linawachanganya wateja.

Baada ya Keds Tanzania kufungua shauri lao Novemba 7, FCC ilitoa notisi ya kuzuia kuuzwa kwa sababu za Mo Cleansoft ambazo zilizuiwa kwenye maghala mbalimbali ya Buguruni na Mbagala wakati shauri hilo likisikilizwa.

Kwa mujibu wa nyaraka za uamuzi wa FCC ambazo Mwananchi imeziona, FCC imebainisha kwamba mwonekano wa sabuni hizo mbili unafanana, jambo ambalo linaweza kuwachanganya watumiaji wa bidhaa hizo.

“Tuna uhakika hata msikilizaji aliye makini hawezi kutofautisha majina hayo mawili yanapotamkwa,” inasema sehemu ya uamuzi wa FCC kama ulivyosainiwa na mwenyekiti wa kamati ya usikilizaji, Josephat Mkizungo.

Akizungumzia suala hilo, mwanasheria wa Keds, Lusajo Mwakalundwa alisema FCC imeamua kwamba sabuni ya Mo Cleansoft ni bandia na shehena iliyozuiwa Novemba 7 inatakiwa kuteketezwa.

“Tutaingia sokoni kukagua kama sabuni za Mo Cleansoft zinapatika. Zile tutakazozikuta zitatakiwa kuteketezwa kwa sababu ni bidhaa bandia,” alisema Mwakalundwa.

Mwanasheria huyo alisema wataenda mahakamani kuzuia uzalishaji wa Mo Cleansoft.

Aliwataka watumiaji wa bidhaa yao ya Kleesoft kuwa makini wanapotaka kununua sabuni hiyo kwa sababu inafanana kwa kiasi kikubwa na sabuni ya Mo Cleansoft.

Chanzo: mwananchi.co.tz