Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume ya Madini yapitisha maombi mapya 7596

Madini Pic Data Tume ya madini yapitisha maombi mapya 7596

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMISHNA wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma amesema kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023-2024 (kuanzia mwezi Julai hadi Septemba), Tume imeidhinisha maombi mapya ya leseni za madini 7596 ikiwa ni asilimia 100 ya maombi yaliyowasilishwa kama mkakati wa kuendelea kutoa fursa zaidi za uwekezaji katika Sekta ya Madini, wananchi kunufaika na Serikali kupata mapato yake.

Prof Mruma ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2023 kwenye Kikao cha Tume jijini Dodoma chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa za utendaji wa Tume kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula, Makamishna wa Tume, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba na menejimenti ya Tume ya Madini.

Amesema kuwa, kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara kupitia ziara, makongamano, warsha na maonesho mbalimbali sambamba na kuongezeka kwa kasi ya uchakataji wa maombi ya leseni mbalimbali za madini.

Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo amefafanua kuwa elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini imeendelea kutolewa sambamba na matumizi ya mfumo wa usimamizi wa ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii kwa wadau wa madini nchini.

Aidha, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2023, Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 184.53 na kusisitiza kuwa Tume kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa imeendelea kuweka mikakati kabambe ili kuhakikisha lengo ililopewa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882.12 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023-2024 linafikiwa.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesisitiza umuhimu wa kufuatilia madeni ya leseni za madini ambazo hazijalipiwa na watumishi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Tume.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live