Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume ya Madini yajivunia uvukaji malengo

A163375eae4a04d681bd19d606e928f3 Tume ya Madini yajivunia uvukaji malengo

Wed, 28 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TUME ya Madini Tanzania imepata mafanikio makubwa kwa miaka miwili mfululizo kwa kuvuka malengo yaliyowekwa na wizara kwa kukusanya maduhuli zaidi ya asilimia 100.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Idrisa Kikula alieleza mafanikio hayo kwenye mkutano wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Sekta ya Madini uliofanyika jijini hapa jana.

Profesa Kikula alisema, Tume hiyo yenye wafanyakazi 68 imevuka malengo katika kukusanya maduhuli mwaka 2018/19 na 2019/20 yaliyowekwa na wizara ambapo katika 2018/19 ilikusanya maduhuli ya Sh bilioni 346.78 sawa na asilimia 101.59 na kuvuka lengo la kukusanya Sh bilioni 310.32.

"Pia katika 2019/20, Tume hii imevuka lengo kwa kukusanya Sh bilioni 528.24 sawa na asilimia 112.31 ya lengo la kukusanya sh bilioni 470.35," alisema.

Pia tume hiyo inaweza kuvuka lengo kwa mwaka wa tatu mfululizo, kwani kwa miezi 10 tangu Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, tayari imekusanya maduhuli ya Sh bilioni 445.2 sawa na asilimia 84 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 526.7 huku bado miezi miwili ikibaki kumaliza mwaka wa fedha.

Profesa Kikula alisema, tume hiyo pia imeongeza idadi ya masoko na vituo vya kuuzia madini kutoka masoko 31 na vituo 38 katika mwaka 2019/20 hadi masoko 39 na vituo 50 hadi Aprili, mwaka huu.

Pia Tume hiyo imeongeza idadi ya utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji madini ambapo 2019/20 ilitoa leseni 5,935 na tangu Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, imetoa leseni za utafutaji na uchimbaji madini 8,709.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akifungua mkutano huo alisema wizara hiyo inatambua mchango mkubwa wa tume hiyo katika kuhakikisha raslimali ya madini inawanufaisha watanzania na taifa kwa ujumla.

Profesa Msanjila aliipongeza tume hilo kwa kuongeza ukusanyaji maduhuli na kuvuka malengo kila mwaka ambako kumesaidia kuongeza pato la taifa kutoka 3.4 katika mwaka 2018/19 hadi asilimia 6.4 Desemba mwaka jana.

Profesa Msanjili alisema hakuna shaka kutokana na mchango mkubwa wa tume, sekta hiyo itakua zaidi na hadi watafikia ndoto ya asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Naye Kamishna wa Tume, Profesa Abdulkarim Mruma aliomba ushirikiano zaidi uendelee ili tume iendelee kupata mafanikio zaidi kwa manufaa ya watanzania na taifa kwa ujumla.

Chanzo: www.habarileo.co.tz