Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume ya Madini yaidhinisha maombi 7,800 ya leseni

20849 Madini+pic TanzaniaWeb

Sat, 6 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Tume ya Madini imeidhinisha maombi 7,879 ya leseni mbalimbali za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini ili kupelekwa kwenye mamlaka husika ambayo ni Baraza la Mawaziri ambapo kati ya hizo, leseni za uchimbaji ni 14.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewaambia waandishi wa habari leo jijini hapa kuwa leseni hizo zimeidhinishwa baada ya tume kukutana Septemba 25, 2018 ili kupokea na kujadili taarifa za kamati za tume na utekelezaji wa kazi katika kipindi cha mwezi Mei hadi Septemba mwaka huu.

Amesema kuwa katika leseni hizo, leseni za utafutaji wa madini (prospecting license) ni 263, leseni kubwa (special mining license) ni tatu, leseni za uchimbaji wa madini (mining license) 14, pamoja na leseni moja ya sihia (transfer) ya uchimbaji wa kati.

“Leseni hizo za uchimbaji zimetolewa ili kutekeleza uchimbaji huo kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Mbeya, Geita, Dar es salaam, Mara na Morogoro,” amesema Profesa Kiula.  

“Lakini pia kuna leseni za uchimbaji mdogo (primary mining license) ambazo ziko 6313, leseni za uchenjuaji wa madini (processing license) ziko nane, pia kuna leseni za biashara ya madini hapa kuna leseni kubwa 557 na leseni ndogo 720,” amesema Profesa Kikula.

Profesa Kikula amewataka wale wote wenye leseni hizo kufuata taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao kulingana na maelekezo yanavyowataka na si vinginevyo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa leseni Tume ya Madini, Profesa Terence Ngole amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo kuvamia maeneo ya wawekezaji tayari maeneo 76 yamerasimishwa kwa ajili ya wachimbaji hao wadogo.

“Hii itatusaidia katika kuhakikisha kuwa hakuna muingiliano katika maeneo ambayo wawekezaji walishapatiwa kwa ajili ya kuchimba, lakini pia itawafanya wachimbaji hao wadogo wadogo kuwa na maeneo maalumu ya kufanya shughuli zao bila kuingiliana,” amesema Profesa Ngole.

Chanzo: mwananchi.co.tz