Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume ya Madini na TRA kukusanya mapato ya madini (+picha)

WhatsApp Image 2021 03 12 At 11.22.32 1 660x400.jpeg Tume ya Madini na TRA kukusanya mapato ya madini (+picha)

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: millardayo.com

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka mikakati ya kushirikiana kwa pamoja kwenye Sekta ya Madini ili iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Uchumi wa Nchi.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo katika kikao kati ya Tume ya Madini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Da es Salaam chenye lengo la kuangalia namna ya utekelezaji wa makubaliano kati ya TRA na Tume ya Madini ya utendaji kazi kwenye Sekta ya Madini ambayo yalisainiwa Septemba, 2020.

Amesema kuwa, ushirikiano kati ya Tume ya Madini na TRA utarahisisha usimamizi kwenye Sekta ya Madini hususan kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa kubadilishana taarifa za kodi mbalimbali zinazolipwa Serikalini.

Katika hatua nyingine akielezea mikakati ya Tume ya Madini kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021-2022, Mhandisi Samamba amesema Tume imeweka lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 600 na kuongeza kuwa lengo ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unakua na kufikia asilima 10 ifikapo mwaka 2025.

“Kama Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, menejimenti, maafisa madini wakazi wa mikoa na maafisa migodi wakazi tumeweka mikakati  mbalimbali ya kuhakikisha kasi ya  ukusanyaji wa maduhuli inazidi kuimarika,” Mhandisi Samamba.

Katika hatua nyingine alimshukuru Waziri wa Madini, Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kwa msaada kwenye utatuzi wa changamoto mbalimbali.

Wakati huo huo akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki alisema kuwa tangu kuanzishwa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini mapema Machi, 2019 Serikali ilipata kiasi cha shilingi bilioni 211.2 ikiwa ni kama mrabaha na kodi ya ukaguzi kupitia masoko ya madini yaliyopo kila mkoa wa Madini.

Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini hali ya ukusanyaji wa maduhuli imeendelea kuimarika nchini kwa kuwa wachimbaji wadogo wa madini wameanza kuwa na uelewa wa umuhimu wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini.

Akielezea manufaa ya masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa alisema kuwa wachimbaji wadogo wa madini wanapata bei elekezi zinazoendana na soko la dunia na kufanya biashara ya madini kuwa na  faida.   “Zamani wachimbaji wadogo walikuwa wakifanya biashara ya madini kwa hasara kwa kuwa walikuwa wanadhulumiwa, lakini tangu masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini yameanzishwa, wachimbaji wadogo wameanza kuyatumia kwa kuuza madini yao kulingana na bei elekezi inayoendana na Soko la Dunia inayotolewa na Tume ya Madini na kulipa kodi mbalimbali Serikalini,” Kasiki

Katika hatua nyingine, Kasiki aliongeza  manufaa mengine kuwa ni pamoja na kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli kwa Serikali ambayo yanatumika kuendeleza Sekta nyingine.

Kikao hicho kilichoongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kilihusisha watendaji kutoka Tume ya Madini, watendaji kutoka TRA wanaotoka katika Idara za walipa kodi wakubwa, walipa kodi wa kati na forodha ambacho lengo lake lilikuwa ni kujenga uelewa wa pamoja wa watendaji wa Tume ya Madini na TRA kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji na kuzipatia ufumbuzi.

Chanzo: millardayo.com