Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume ya Madini kukusanya bil 650/-

6029b0823332c87c04d9eb98d9f0b090 Tume ya Madini kukusanya bil 650/-

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Madini kupitia Tume ya Madini katika mwaka wa fedha 2021-2022 inatarajia kukusanya shilingi bilioni 650 na kuendelea kuboresha shughuli za uchimbaji na madini.

Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo aliyasema hayo jana mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi kilichokutanisha wahasibu kutoka Tume ya Madini makao makuu na ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa.

Tarimo alisema Tume ya Madini imeweka mikakati kwenye usimamizi wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza udhibiti utoroshaji wa madini, usimamizi zaidi kwenye masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini.

Alisema tume hiyo pia itaboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha kuna vitendea kazi vya kutosha kwenye ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa na masoko ya madini.

Tarimo alisema kati ya Julai, 2020 hadi Februari mwaka huu Tume ya Madini ilikusanya shilingi bilioni 399 ikiwa ni sawa na asilimia 113.7 ya lengo la kipindi husika ambalo lilikuwa kukusanya shilingi bilioni 351.

Aliwataka wahasibu waendelee kuwa wabunifu kwenye utendaji kazi na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto katika kukusanya maduhuli ili kuhakikisha sekta inazidi kukua na ikifika mwaka 2025 iwe na mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa.

Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, William Mtinya alisema lengo la kikao hicho ni kuwapa wahasibu uelewa kuhusu usimamizi wa sekta ya madini hususan kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa kutumia mifumo mbalimbali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz