Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumbaku yote Urambo kununuliwa

57015 Pic+tumbaku Tumbaku yote Urambo kununuliwa

Sat, 30 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMPUNI ya ununuzi wa tumbaku ya Alliance One imekubali kununua kilo 705,474 za tumbaku ya msimu uliopita ya vyama 10 vya ushirika (AMCOS), wilayani Urambo, mkoani hapa.

Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wilayani humo, Absama Kajuna alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya zao hilo katika mkutano wa wadau wa kilimo.

Alisema tumbaku hiyo maarufu kama makinikia, sasa itanunuliwa kwa bei ya Sh. 1,265 sawa na dola za kimarekani 0.55 kwa kila kilo moja, jumla Sh. 892,474,610.

“Nafurahi kuwajulisha kuwa tumbaku yote iliyokosa soko mwaka jana ya vyama 10 vya msingi sasa itanunuliwa na kampuni ya Alliance One, ila haitakuwa na madaraja, itachukuliwa kwa bei moja tu,” alisema.

Mkuu wa wilaya hiyo, Angelina Kwingwa, alibainisha kuwa kitendo cha kuchelewa kwa ununuzi ya zao hilo mwaka jana, kilichangia tumbaku hiyo kutonunuliwa yote jambo ambalo limewasababishia hasara wakulima.

Alisema upungufu uliojitokeza mwaka jana kwa kampuni ya Magesa kuwa imekosa usafiri wa kubebea tumbaku yote wakati mkataba ulikuwa umeshafungwa hayakubaliki.

Alisisitiza kuwa mkataba wa ununuzi ukishafungwa masuala ya usafiri sio jukumu la mkulima ni juu ya mnunuzi mwenyewe na kuonya kitendo hicho kikijirudia kampuni itawajibika kwa hasara itakayotokea.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Adam Malunkwi, alisema kama kampuni hiyo imekubali kununua tumbaku hiyo iliyosalia msimu uliopita, waichukue mara moja badala ya kuiacha kwenye maghala.

Alisisitiza kuwa kuanzia sasa Bodi ya Tumbaku Tanzania haitatoa leseni kwa kampuni yoyote ya ununuzi ambayo haitakuwa imekidhi vigezo.

Kaimu Mkurungezi wa Bodi hiyo, Stanley Mnozya, alisema kwamba kutokana na ununuzi huo, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo itapata ushuru wa Sh. 26,774,238 na vyama vya msingi kupitia chama kikuu cha wakulima kitapata Sh. 44,621,230.

Alisema ununuzi huo umesaidia wakulima wa tumbaku kupata pesa kwa kuwa bila jitihada za bodi hiyo kufanya ushawishi tumbaku hiyo ili kuwa iendelea kubaki kwa wakulima kitu ambacho kingesababisha kutupwa.

Aliwataka wakulima wenye tumbaku ndani wazipelekea kwenye magahala ili ziweze kununuliwa kwa kuwa hadi sasa kampuni ya ununuzi wa tumbaku zinahitaji tumbaku hizo za msimu ulipita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live